Na Yohane Gervas, Rombo
WANANCHI wilayani hapa wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kufichua wahalifu
katika jamii zao ili waweze kupunguza vitendo vya uhalifu vinavyofanywa katika maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Rombo kwani suala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila Mtanzania na si suala la polisi tu.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mashati, Yasinti Shinyaka wakati alipokuwa akihutubia wakazi wa Kijiji cha Keni-Mashati katika Mkutano Mkuu wa Kijiji hicho uliofanyika leo.
Shinyaka amesema kuwa wahalifu wapo katika jamii zao na wanafahamika hivyo akawataka wakazi hao kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha kuwabaini wahalifu
hali ambayo itawafanya wananchi waishi kwa amani.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Damas Merinyo, amewataka wakazi wa kijiji hicho cha Keni-Mashati kuhudhuria mikutano ya kijiji pindi wanapohitajika ili waweze kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo yao badala ya kulalamikia vijiweni.
Amesema kuwa wapo baadhi ya watu ambao hawahudhurii kwenye mikutano na vikao vya kijiji na badala yake wanabakia nyumbani na kulalamika vijiweni hali ambayo inasababisha uduni wa maendeleo katika jamii zao.