Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi nchini limeandaa hafla maalumu ya kumuaga IGP Mstaafu Said Mwema inayotarajia kufanyika Februari 15 kuanzia majira ya saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana katika viwanja vya Polisi Barracks, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso-SSP alisema katika hafla hiyo kutakuwa na mambo mbalimbali yaliyoandaliwa ikiwemo gwaride maalum la heshima kwa ajili ya kumuaga kiongozi huyo mstaafu wa polisi.
“…Napenda kuufahamisha umma kuwa, mnamo tarehe 15/02/2014 siku ya Jumamosi katika viwanja vya Polisi Barracks, barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam, kutakuwa na hafla ya kumuaga IGP Mstaafu Said Alli Mwema kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana,” alisema Senso katika taarifa hiyo.
Alisema katika kipidi cha uongozi wa Jeshi la Polisi, IGP mstaafu, Mwema alishirikiana vyema na wananchi wa kada zote wakiwemo wadau mbalimbali wa amani, hususani katika dhana ya Ulinzi shirikishi na Polisi Jamii; hivyo Jeshi la Polisi nchini kwa kulitambua hilo, litatumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote kuhudhulia hafla hiyo.
Aidha, IGP Mstaafu Said Alli Mwema katika uongozi wake alianzisha na kusimamia mifumo mbalimbali ya kuzuia na kukabiliana na uhalifu hapa nchini ikiwemo maboresho ndani ya Jeshi la Polisi, ili kuhakikisha Jeshi linafanya kazi kwa weledi, usasa na ushirikiano na wananchi.