Jeshi la Marekani laondoka Iraq

Majeshi ya Marekani yakiondoka Iraq

WANAJESHI wa mwisho wa Marekani nchini Iraq wameondoka kabla ya siku ya mwisho wa mwaka 2011, ambao ndio muda uliokubaliwa baina ya Iraq na Marekani jeshi hilo kuondoka.

Taarifa zaidi kutoka Iraq zinasema gari la jeshi la mwisho lilivuka mpaka na kuingia Kuwait asubuhi mapema leo, na kumaliza vita vya Iraq vya karibu miaka 9.

Msafara wa mwisho wa matingatinga takriban 110 uliwasili Kuwait, ukishangiliwa huku wanajeshi wakikumbatiana. Msafara huo ulikuwa na wanajeshi 500 wa mwisho wa Marekani kuondoka Iraq.

Katika vita vya Iraq Marekani ilipoteza karibu wanajeshi 4500 huku zaidi ya 30,000 wakijeruhiwa. Inakisiwa raia zaidi ya 100,000 wa Iraq waliuwawa, na haijulikani wangapi wameachwa na vilema katika milipuko inayotokea nchi hiyo.

Sasa Wamarekani wanaondoka, lakini Marekani itaendelea kuwa na madaraka kupitia ubalozi mkubwa ambao utakuwa pia na maofisa wa kijeshi 150 wataoshughulikia biashara ya silaha kwa Iraq; pamoja na raia zaidi ya 100 kuwafunza wanajeshi wa Iraq namna ya kutumia vifaa vya Marekani.
-BBC