JESHI la Magereza nchini Tanzania limesema taarifa zinazotolewa kupitia ujumbe mfupi wa simu na baadhi ya watu kuwa Nguza Vicking au maarufu kama Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza maarufu kama Papii Kocha wameachiwa huru kutoka gerezani ni za uzushi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Jeshi la Magereza, Mkaguzi, Lucas Mboje alisema wafungwa hao wawili wanaotumikia kifungo cha Maisha gerezani, bado wanaendelea kutumikia adhabu zao na kuwataka wananchi wasipotoshwe na uzushi huo mkubwa uliolenga kulichafua jeshi hilo.
“Hivi sasa kuna taarifa zimesambaa kupitia Ujumbe mfupi wa simu(SMS) na mitandao ya kijamii zikihusisha kuachiliwa huru kwa wafungwa wawili wanaotumikia Kifungocha Maisha gerezani. Wafungwa hao wanaotajwa ni Nguza Vicking(Maarufu kwa jina Babu Seya) na Johnson Nguza(Maarufu kwa jina la Papii Kocha).”
“…Napenda kuufahamisha Umma wa Watanzania kuwa taarifa hizo zote zilizotolewa kupitia njia hizo ni za Uongo na uzushi mkubwa na zinalenga kuipotosha jamii kwani wafungwa hao wapo gerezani na wanaendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha Maisha gerezani kwa mujibu wa Sheria,” alisema Lucas Mboje katika taarifa yake.
Aidha aliongeza kuwa Jeshi la Magereza limetoa onyo kali kwa watu kujiepusha na uhalifu huo na linawataka wale wote wanaotumiwa ujumbe wa aina hiyo waepuke kuusambaza ujumbe huo kwa watu wengine bali waufute, kwani kuendelea kuusambaza ni kosa kisheria.
Alifafanua kuwa Jeshi la Magereza linaendelea na uchunguzi wa kina ili kuwabaini wanaosambaza ujumbe huo likishirikiana na Vyombo vingine muhimu kwa lengo la kuwakamata wahalifu waliosambaza ujumbe hui ili mkondo wa Sheria uchukue nafasi yake.