Jengo la Ghorofa 16 Laporomoka na Kuua Dar es Salaam

Waokoaji wakiubeba maiti ya mmoja wa watu waliobomokewa na jengo hilo.

Kifusi cha ghorofa hilo kama kinavyoonekana kwenye picha

Baadhi ya waokoaji wakikata nondo za zege kutafuta njia ya kuingia ili kuokoa wa

Kazi ya uakoaji ikiendelea kwa kufukuwa kifusi

gari lililofukiwa na kifusi likibebwa na winchi

Baadhi ya askari na vikosi mbalimbali wakijipanga kuondoa kifusi

Jengo la Ghorofa 14 ambalo nalo linajengwa na kampuni iliyokuwa ikijenga ghorofa lililoporomoka, ambalo nalo limezuiwa kuendelea na ujenzi

Na dev.kisakuzi.com

JENGO la ghorofa 16 lililokuwa likiendelea na ujenzi eneo la makutano ya mtaa wa Hindilaghandi na Zanaki jijini Dar es Salaam limeporomoka ghafla leo majira ya saa mbili asubuhi na kufukia baadhi ya watu. Kwa mujibu wa taarifa ambazo mwandishi wa habari hizi amezipata kutoka kwa baadhi ya mashuhuda waliokuwa jirani na jengo hilo, inasemekana kuna zaidi ya watu 60 ambao wanadaiwa kufukiwa katika jengo hilo wakiwemo watoto ambao walikuwa wakicheza mpira jirani na jengo hilo.

Mtandao huu umeshuhudia miili ya watu wanne ambao wameopolewa katika kifusi wakiwa tayari wamekufa na juhudi za kuwatafuta watu zaidi katika kifusi cha zege zikiendelea. Watu 16 wamejeruhiwa baada ya kuanguka kwa jengo hilo na wanaendelewa kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Vikosi vya uokoaji kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Msalaba Mwekundu, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kikosi cha Zimamoto na kampuni mbalimbali binafsi vinaendelea kutafuta miili ya watu ili kuwaokoa ama kupata maiti kwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Hadi majira ya saa tano mchana baadhi ya ndugu za watu ambao walikuwa wamefukiwa na kifusi walikuwa bado wakifanya mawasiliano wakiomba msaada wa kuokolewa na juhudi za kupangua kifusi zilikuwa zikiendelea ili kuwanusuri waathirika hao. Hata hivyo kadri ya muda ulivyokuwa ukiendelea mawasiliano yalikatika na simu kupoteza mawasiliano.

Hata hivyo changamoto kubwa ilikuwa ni namna ya kupatikana vifaa vya kisasa vya uokoaji jambo ambalo lilionekana kikwazo cha kasi ya uokoaji. Vifaa vilivyokuwa vikitumika ni magari ambayo hutumika katika ujenzi wa barabara maarufu kama vijiko pamoja na winchi. Hadi dev.kisakuzi.com inaondoka eneo la tukio majira ya saa kumi na moja, zoezi la uokoaji lilikuwa likiendelea na tayari Rais Jakaya Kikwete, Makamo wa Rais, Dk. Gharib Bilal, baadhi ya mawaziri na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam walitembelea eneo la tukio kujionea hali halisi na zoezi la uokoaji.

Taarifa zaidi ambazo mtandao huu umezipata kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa jengo lililoporomoka ni kwamba hii ni mara ya pili ajali ya kuporomoka kwa kifusi ndani ya jengo hilo kutokea, kwani walisema zege ya ghorofa ya 16 pekee iliporomoka tena hivi karibuni kabla ya mafundi kuanza tena ujenzi wake kwa mara ya pili.

Tayari Rais Kikwete amezuia kuendelea kwa ujenzi wa jengo lingine la ghorofa 15 ambalo lipo jirani na jengo hilo, ambalo nalo linadaiwa kujengwa na Mkandarasi aliyekuwa akijenga jengo lililoporomoka. Taarifa zinasema tayari jengo hilo nalo limeanza kuonesha nyufa katika ghorofa ya nne, hivyo kuleta wasiwasi kwa majirani eneo hilo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema tayari jeshi hilo linawahoji waandisi wa Manispaa ya Ilala ili kupata taarifa za kina za ujenzi wa jengo hilo. Jengo hilo lilikuwa likijengwa na Kampuni ya Lucky Consruction Limited ya jijini Dar es Salaam.