RAIS wa Marekani Barack Obama juzi amemteua Jenerali David Petraeus, kamanda wa majeshi ya kigeni nchini Afghanistan kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA).
Obama amechukua hatua hiyo huku akijiandaa kufanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri kabla ya uchaguzi mkuu wa rais mwaka 2012.
Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa mkurugenzi wa CIA, Leon Panetta anatarajiwa kuwa waziri wa ulinzi kuchukua nafasi ya Robert Gates anayestaafu mwishoni mwa Juni mwaka huu.
Nafasi ya Jenerali Petraeus itajazwa na Luteni Jenerali John Allen wa jeshi la majini.
Baraza la Seneti litapaswa kuthibitisha mabadiliko hayo.
Akitangaza mabadiliko hayo katika nyadhifa za juu za maofisa wa usalama, Obama pia alimteua Ryan Crocker kuwa balozi ajaye wa Marekani nchini Afghanistan.
‘Hawa ni viongozi niliowachagua kusaidia kutulinda kipindi kigumu kijacho,” Obama alisema huku Gates, Panetta, Jenerali Petraeus wakiwa wamesimama pembeni yake Ikulu mjini hapa.
Hata hivyo, kuondoka kwa Petraeus kunazua maswali juu ya hali ya baadaye ya vita visivyopendelewa na wengi vya karibu muongo mmoja nchini Afghanistan.
Wachambuzi wa mambo wanahofia kuondoka kwake kunaweza kuvuruga hatua za maendeleo zilizofikiwa na kuvunja nguvu juhudi za nchi hii kuimarisha ushirikiano na Pakistan.