MITI ya michungwa inahitaji uangalizi wa hali ya juu, kitu ambacho wakulima wengi ama hawakijui ama hawakitilii maanani.miti hii hupandwa kwa mbegu za milimao ya kawaida (rough lemon) halafu inaungwa kwa kutumia vikonyo maalumu vya michungwa.
Miti hii inahitaji ukaguzi wa mara kwa mara ili kupunguza matawi yanayokuwa bila mpangilio kwani matawi haya huzuia mti kupata hewa kwenye shina. Matawi haya ni pamoja na:-
• Matawi yenye magonjwa, matawi haya huondolewa ili kuzuia ugonjwa usienee katika matawi ama mimea mingine.
• Matawi yaliyokufa au matawi yaliyokauka,
• Matawi makubwa kuliko mengine na yanayoenda juu sana, matawi haya huwa makubwa sana na hivyo kunyonya maji mengi ya mmea matawi haya yanaweza kutoa machungwa lakini machungwa yake huwa hayana maji kwani maji mengi hunyonywa na tawi.
• Matawi yanayoota kuelekea kwenye shina, Matawi haya huzuia shina kupata hewa hivyo husababisha ugonjwa wa ukungu kwa mmea
• Matawi madogo madogo yanayoota katika tawi moja haya huondolewa kwani yanasababisha mmea kuwa kama kichaka ambapo hewa na mwanga havifiki kirahisi kwenye shina
Kupunguza matawi yasiofaa katika mti (plunning) huongeza uhai wa mti na kuongeza uzalishaji kwa asilimia 80%. Zoezi hili la kupunguza matawi linashauriwa lifanyike mara baada ya kuvuna ili kuuandaa mti kwa msimu mpya wa uzalishaji.
Vitendea kazi vya kupunguzia matawi haya ni pamoja na mkasi maalumu wa kukatia matawi madogo na msumeno wa kupunguzia matawi makubwa.
Epuka kutumia panga kwani linaacha kovu kwenye mti, kovu hili huweza kusababisha ugonjwa wa Gumosisi yaani mti kutoa kitu kama gundi katika eneo la kovu.