Wanajamvi, leo tunaingia sehemu ya tatu, na ya mwisho ya makala yetu yenye kichwa cha habari hapo juu. Mara nyingine tena, kama umepitwa na makala zilizotangulia (sehemu ya 1 & 2), basi sio tatizo, wewe ingia kwenye “Popular Posts” hapo mkono wa kulia na utaziona zote. Tukirudi kwenye mada, Ziglar anaendelea kusema kwamba mtu anayeishi maisha bora, anajua (au anafanya) yafuatayo:
11) Anawapenda wasiopendeka, anawapa matumaini waliokata tamaa, anakuwa rafiki kwa hata wale wasiokuwa na urafiki, na kuwa hamasisha wale waliokata tamaa ya maisha kwa ujumla.
12) Ni mrahisi kusamehe yaliyopita, na kuganga ya jayo (kwa ufupi unaishi maisha chanya na si hasi).
13) Anaelewa (au unaelewa) kwamba mkubwa kuliko wote katika jamii ni yule mtumishi mkuu wa jamii husika. Hivyo basi, kwa maneno mengine unafahamu kwamba cheo (au utajiri) ni dhamana, na hautumii cheo hicho au pesa hizo kudhalilisha na kunyayasa wengine. Embu pata picha hapa kama viongozi wetu wa leo, matajiri, au watu maarufu wa leo katika jamii zetu wangekuwa wanafahamu hili na kuzingatia hali ingekuwa aje? Bila shaka tungekuwa na jamii bora zaidi.
14) Unatambua, unakubali, unaendeleza, na kutumia vipaji ulivyojaaliwa na Mungu kwa ajili yake, na kwa faida ya binaadam wenzio kwa ujumla (na sio kwa faida yako binafsi tu).
15) Mwisho, mwisho wa siku (tutakapofikwa na umauti, na kama tumeishi kwa misingi iliyoanishwa hapo juu), tutakuja kusimama mbele ya Mungu, na yeye atasema “Kazi nzuri! wewe ni mtumishi mzuri na muaminifu”, Ziglar ana malizia kusema.
Wanajamvi, nami namalizia kwa kusema, tuzingatie misingi hii, na chaguo libaki kwetu kuifuata au kuipuuza. Chaguo linabaki kwetu kuishi maisha bora au bora maisha…..
Asanteni, na tukutane kwenye mada nyingine.
Rungwe Jr.