Wanajamvi wa Chuo Cha Maisha natumai wote mnaendelea vema. Leo tupo katika sehemu ya pili ya mtiririko wa zile sifa 15, ambazo mtaalam Ziglar ametuwekea bayana kwamba ndio zitatusaidia kutambua kama tunaishi maisha bora au bora maisha. Leo tunaendelea na sifa nyingine 5, kwani wiki iliyopita tulizitaja 5, na kama ulipitwa, basi gonga hapa: http://www.thehabari.com/habari-tanzania/je-unaishi-maisha-bora-au-bora-maisha; chap chap, ili uzisome kabla ya kuendelea.
Leo Ziglar anaendelea kwa kusema…unaishi maisha bora (Over the Top), kama:
6) Unajua kwamba kushidwa kusimamia kilichosahihi kimaadili, ndio chanzo cha kuwa mhanga wa yale yaliyokuwa makosa ya kijinai. Kwa mfano kama wewe ni baba au mama kwenye nyumba na umeshindwa kuwalea watoto wako kimaadili kwa kuwahimiza mema na kuwakataza mabaya, uwezekano ni mkubwa kwamba watoto hao watakuja kuwa na matendo ya hovyo hovyo katika jamii (kama wizi, utumiaji wa madawa ya kulevya, na nk). Mtoto akija kuwa mwizi haoni hatari kuja hata kukuibia na wewe nyumbani. Je haujawa mhanga wa udhaifu wako mwenyewe wa kushindwa kukemea maovu na kuamrisha mema?
7) Umeridhika na ulivyo na ulichonacho, hivyo basi una imani na Mungu na una shirikiana na binaadam wenzio (bila kinyongo na tamaa).
8) Umeweza kuwa rafiki kwa maadui zako, na umejijengea heshima miongoni mwa wale wanaokufahamu vizuri (kumbuka, ni rahisi kufeki na kuwarubuni wale wasiokufahamu vizuri).
9) Unaelewa kwamba watu wengine wanaweza wakakupa raha/furaha (kwa kukufanyia mambo), lakini raha/furaha ya kweli upatikana pale unapowafanyia mambo watu wengine.
10) Ni mpole kwa wenye visirani, muungwana kwa wasio na adabu, na mkarimu kwa wasiojiweza.
Wanajamvi, tukutane tena hapa, na tutaendelea kuhabarishana hizo sifa/ nguzo nyingine zilizobaki kutoka kwa mtaalam wetu Zig Ziglar.
Rungwe Jr.