SHULE ya Sekondari ya Mabibo iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni imesaini Mkataba wa Mradi wa ujenzi wa Maabara ya Kisasa unaojulika kwa jina la “Grassroot Human Security” ambao utagharimu kiasi cha USD 118,873 ambazo ni takribani mil 193 za Kitanzania.
Mradi huo umesainiwa leo jijini Dar es Salaam kati ya Balozi wa Japani Nchini Tanzania, Masaki Okada mbele ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda na Mkurugenzi wa Manispaa Mwandisi Mussa Natty.
Kwa pamoja Meya wa Kinondoni, Mwenda na Mkurugenzi Natty wameshukuru Serikali ya Japani kwa msaada huo na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa nchi hiyo na kuhimiza watoto wapende masomo ya sayansi na kuifanya Kinondoni iwe juu kielimu.
Kwa upande mwingine balozi Masaki amewataka Watanzania kuwekeza Kwenye sayansi na teknolojia kuliko kutegemea kununua kwa ajili ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini vile vile amewashukuru Bi. Bernadetha Thomas na Omath Sanga Maofisa elimu wa Manispaa kwa kuibua mradi huo.