JAPAN imekubali kuangalia uwezekano wa kugharimia ukarabati na
uboreshaji mkubwa wa Reli ya Kati na pia imekubali kuwa mbia mkuu
katika kuiwezesha Tanzania kuleta mageuzi makubwa katika kilimo cha
mpunga kwa nia ya kuzalisha mchele zaidi na kujitegemea kwa zao hilo
muhimu la chakula.
Serikali ya Japan imeeleza msimamo huo wa kuisaidia Tanzania katika
maeneo hayo baada ya kuombwa rasmi kufanya hivyo wakati wa mazungumzo
rasmi kati ya Tanzania na Japan kati ya Rais wa Jamhuri ya Muuungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Japan,
Mheshimiwa Shinzo Abe.
Aidha, Japan imeombwa na kukubali kuangalia uwezekano wa kugharimia ujenzi wa reli mpya kutoka Tanzania kwenda nchi za Rwanda, Burundi na hatimaye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Tanzania pia imeiomba Japan kuwa mshirika kiongozi katika mageuzi ya
kilimo cha mpunga katika Tanzania ili kuwezesha kuongeza usalama wa
chakula na hasa wa mchele kwa Tanzania na majirani zake.
Tanzania vile vile imeiomba Serikali ya Japan kuyashawishi makampuni
makubwa ya nchi hiyo kuwekeza katika uchumi wa Afrika kwa sababu Bara
la Afrika linaendelea kuwa soko muhimu la bidhaa za viwandani za
Japan.
Maombi hayo yametolewa leo, Alhamisi, Mei 30, 2013 na Mheshimiwa
Kikwete wakati alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Mheshimiwa
Abe, mjini Tokyo ikiwa sehemu ya shughuli za Rais Kikwete katika ziara
ya kikazi ya siku saba katika Japan.
Katika mazungumzo hayo ofisini kwa Waziri Mkuu, Rais Kikwete ameiomba Japan kufikiria kuiunga mkono Tanzania kwa kugharimia ukarabati na uboreshaji wa Reli ya Kati kutoka reli nyembamba ya sasa kuwa reli ya
kiwango kinachokubaliwa kimataifa.
Aidha, Rais Kikwete ameiomba Japan kuangalia uwezekano wa kugharimia ujenzi wa reli mpya kutoka Isaka, Tanzania kwenda Kigali, Rwanda na hatimaye Burundi na DRC.
“Waziri Mkuu, reli yetu ya kati ni nzee sana na tunataka
kuboresha reli yenyewe kwa kuibadilisha na kuifikisha kiwango cha
kimataifa na pia kukarabati karakana zote muhimu za kuhudumia reli
hiyo. Aidha, tunashirikiana na Rwanda, Burundi na DRC kujenga reli
mpya kwa sababu nchi zote hizi zinategemea Bandari ya Dar es Salaam
kupitisha mizigo yao,”
Ameongeza: “Tumekamilisha upembuzi yakinifu na michoro kwa msaada wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na kampuni moja ya Barrington Santa Fe ya
Marekani na sasa tunatafuta mbia wa kugharimia ujenzi wake.”
Kuhusu uboreshaji wa kilimo cha mpunga, Rais Kikwete
amemwomba Waziri Mkuu Abe kuifanya Japan kuwa mbia kiongozi katika
kilimo cha mpunga ili kuiwezesha Tanzania kujitegemea kwa mchele na
hata kuweza kulisha nchi za jirani.
“Katika kilimo, tunalenga kujitosheleza kwa mahindi na mchele. Tunao
wabia wachache lakini tunataka Japan iwe mbia kiongozi kwa sababu ya
uzoefu wetu katika kilimo cha mpunga. Tunahitaji kuongeza uzalishaji
kwa sababu majirani zetu wanatutegemea.”
Kuhusu Serikali ya Japan kuyashawishi makampuni binafsi ya nchi hiyo
kuwekeza katika Afrika, Rais Kikwete amesema: “Biashara kati ya Japan na Afrika inaongezeka na uwekezaji unaongezeka, lakini tunaweza kufanya zaidi kwa sababu katika kila magari 10 kwenye barabara za Afrika tisa yanatoka Japan. Maduka ya vifaa vya elekroniki yamejaa vifaa na vyombo kutoka Japan – ziwe kamera, ziwe redio, ziwe televisheni lakini hayo makampuni mengi ya
Japan yanawekeza katika Afrika.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Uwekezaji unatunufaisha sana katika Afrika.
Chukua mfano wa Kampuni ya Somitomo – imezalisha vyandarau milioni 30 pale Arusha na ni vyandarua hivyo ambavyo vimepunguza malaria katika
Afrika. Tanzania kwenye malaria imepungua kwa kiasi cha asilimia 60 kwa sababu ya uwekezaji huo.”
Rais pia ameiomba Serikali ya Japan kuisaidia kampuni hiyo ya Somitomo
kuwekeza zaidi katika uzalishaji umeme. Kwa sasa kampuni hiyo
inashirikiana na Serikali kuzalisha megawati 240 katika eneo la
Kinyerezi, Dar Es Salaam.
Rais pia ameomba Japan kuongeza nafasi za shahada ya juu ya PHD katika kufundisha madaktari wa Tanzania na kusaidia kuongeza uwezo wa
Tanzania katika matumizi ya mkongo wa taifa ambao Serikali iliujenga.