Na Joachim Mushi
IDADI ya watia nia ya kugombea nafasi ya urais wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imezidi kuongezeka huku wanaojitokeza wakiendelea kutoa ahadi nono na za kuvutia kwa Watanzania. Jana mgombea January Makamba amejitokeza kutangaza nia ambapo miongoni mwa vipambele vyake ni kutoa huduma bora za afya huku akiahidi kumpatia bima ya afya kila Mtanzania endapo atafanikiwa kupewa nafasi ya Urais wa Tanzania.
Makamba aliyetangaza nia katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam alisema atakuwa na vipaumbele vitano ambapo cha kwanza ni kutoa huduma bora za kijamii ikiwemo afya, elimu maji na huduma nyingine muhimu kwa jamii na kipaumbele cha pili ni kukuza kipato cha Watanzania eneo hili akiangalia kila raia anayetoka jasho lazima anufaike na kazi anayoifanya.
Alisema kipaumbele cha tatu ni kuwa na mfumo wa utawala bora, wa haki na unaofuata sheria huku akijikita katika kujenga upya taasisi za umma zinazosimamia sheria na kuhakikisha kila Mtanzania anafuata sheria na taratibu za nchi. Alisema taasisi zitahakikisha zinakabiliana na aina yoyote ya ubadhilifu na taarifa kama za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali itakuwa ikifanyiwa kazi kwa vitendo na watuhumiwa waliotajwa watakuwa wakiwekwa kando huku wakishughulikiwa kimashtaka kisheria.
Makamba ambaye alionekana kufafanua zaidi namna Serikali atakayoiunda itakavyokuwa ikitatua changamoto zilizopo, aliongeza kuwa kipaumbele cha nne itakuwa ni usimamizi wa uchumi wa nchi huku akiunda vyombo maalumu vitakavyokuwa na mamlaka ya kusimamia uchumi likiwemo Baraza la Uchumi la Taifa litakalokuwa na watendaji wabobefu katika tasnia hiyo na kuwa na vipaumbele mahususi.
Kipaumbele cha tano ni kulinda amani, usalama wa nchi pamoja na mali za Watanzania.Eneo hili Makamba ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mashughuli Mzee Yusuf Makamba alisema kutakuwa na vyombo vya maridhiano na upendo ambavyo vitakuwa vikikutana na mamlaka ya rais kila baada ya miezi miwili kuzungumzia masuala ya usalama, maridhiano na upendo ikiwa ni pamoja na uwepo na jukwaa la amani litakalo kuwa likijadiliana nini cha kufanya juu ya changamoto zinazojitokeza kulinda amani ya taifa kwa ujumla.
Aidha akifafanua zaidi alisema kutakuwa na utaratibu wa kujenga nafasi mahususi za ajira kwa ushirikiano na taasisi binafsi, kujenga chuo kikubwa cha ufundi kwa kila wilaya na kubadili mfumo mzima wa elimu ili kuufanya uzalishe vijana watakaokuwa na uwezo wakujiajiri na si kutegemea ajira pekee. Kauli mbiu ya mwanasiasa huyu kijana ni ‘Tanzania Mpya.
Makamba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, aliongeza kuwa Serikali atakayoiunda itaweka utaratibu wa kutenga kiasi cha shilingi milioni 50 kwa kila kijiji Tanzania ili fedha hizo ziweze kutumika kuwawezesha wanavijiji kuinua shughuli za uzalishaji katika vijiji vyao kwa utaratibu wa kukopeshana.
Alisema sekta ambazo atazitumia kujenga uchumi wa uhakika wa taifa ni pamoja na utalii, madini mbalimbali, bandari, makusanyo ya kodi kiufasaha, kubana matumizi ya Serikali pamoja na sekta ya misitu ambazo zinaweza kuzalisha mapato ya kutosha kuendesha uchumi wa taifa.
“…Nitahakikisha tunafuma na kusuka upya mfumo mzima wa Serikali na utumishi wa uma…Watanzania kumiliki uchumi wao wenyewe na kuwa na nidhamu ya kazi na uwajibikaji. Binafsi sitapata kigugumizi cha kushughulikia hili kwa kuwa sina deni na mtu…,” alisema Makamba akifafanua zaidi.
Hata hivyo wengine waliojitokeza jana kutia nia kuwania nafasi kama hiyo ni pamoja na Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamis Kigwangala na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard K. Membe aliyetangaza nia hiyo kutokea mkoani Lindi.