Na Janeth Mushi, Arusha
WAKAZI wa Jamii ya wafugai wa Kimasai waishio Ukanda wa Afrika Mashariki, Oktoba 21 mwaka huu wanatarajia kuanza sherehe za kuwapeleka jando vijana wa kiume wa jamii hiyo sherehe zinazotarajwia kufanyika katika eneo la elerai katika Manispaa ya Arusha.
Lawasare Langas ambaye ni kiongozi wa jadi na mila za Kimaasai
anayewasilisha jamii ya Olosho, alisema juzi kuwa kabla ya shughuli za
kuwapeleka jando vijana hao wenye umri tofauti, kutafanyika mikesha
miwili katika eneo la Enaboishu wilayani Arumeru kuwaandaa kuanzia
Octoba 18 hadi siku ya tohara.
Kiongozi huyo alisema kuwa kimila wanawapeleka jando vijana wote wa
kiume kila baada ya miaka Saba ambayo ni mwanzo wa rika mpya. Pamoja na tohara, vijana hao pia hupewa mafunzo maalum kuhusu mila na desturi juu ya malezi ya mila, mahusiano kijamii na malezi ya watoto na familia wka jumla.
Kiongozi huyo aliyeongozana na viongozi kadhaa wa mila kwenda kwa
mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye kumwomba asaidie kupatikana ruhusa ya kutumia eneo la mila linalotumika kwa shughuli hiyo ambayo imewekewa uzio na Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA) alisema vijana watakaohusika kwenye tukio hilo wanatoka jamii yote ya Kimaasai kutoka mikoa yote nchini na maeneo ya nchi jirani ya Kenya.
Aidha kundi linalofanyiwa tohara sasa litakalorithi Korianga linaitwa Iltwati. Akizungumza na wazee hao wa mila, Medeye ambaye ni Naibu waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi aliahidi kufuatilia kibali kutoka TANAPA ili shughuli hiyo iweze kufanikiwa ilivopangwa lakini akasisitiza kwamba tohara hiyo lazima iwe kwa ajili ya vijana wa kiume pekee.
Naibu huyo alisema kuwa tohara ni jambo jema na ni mila inayoelekezwa kwa wananume hata kwenye vitabu vitakatifu vya Biblia na Quran, ambapo hata wataalam wa afya wanasema kuwa ingawa haizuii lakini hatari ya maamumbikizi ya virusi vya UKIMWI ni mdogo kwa mwanaume aliyefanyiwa tohara kulinganisha na ambaye hajafanyiwa tohara.
Medeye alisema wahusika pia huelekezwa wajibu wao kwa jamii kiwemo uokoaji wakati wa majanga, ulinzi na ukarimu kwa wahitaji, watoto yatima, wajane na wageni. Medeye alisema kuwa zamani hakukuwa na vikosi vya zima moto katika jamii zetu lakini kila kulipotekea majanga vijana walijitokeza kuokoa kutokana na mbinu na mafunzo waliyopata jandoni, hivyo ni lazima tohara ifanyike kwa vijana wa kiume.
Kwa mara ya mwisho tohara kwa vijana wa Kimaasai ilifanyika Oktoba,
2004 ambapo kundi la vijana walio kwenye rika la Korianga walitahiriwa.