JAN POULSEN AONGEZA WAWILI STARS

Juma Jabu ni mmoja wa wachezaji aliyeitwa katika kikosi hicho.

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen amewaita kwenye kikosi hicho wachezaji Juma Jabu kutoka Simba na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ wa Azam FC kwa ajili ya mechi ya kirafiki inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana mjini Dar es Salaam na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura ni kwamba; wachezaji hao wameitwa kuchukua nafasi za Amir Maftah wa Simba na Nurdin Bakari wa Yanga ambao ni majeruhi.

Wambura amefafanua katika taarifa hiyo iliyotumwa kwenye gazeti hili tando kuwa, mechi ya FIFA dhidi ya Sudan ‘Nile Crocodile’ itafanyika Agosti 10 mwaka huu jijini Khartoum na timu inatarajiwa kuondoka Agosti 8 mwaka huu kwenda huko.

Stars hivi sasa inaendelea na mazoezi Uwanja wa Karume, Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi hiyo ambayo ni moja ya maandalizi kabla ya Septemba 3 mwaka huu kuivaa Algeria ‘Desert Warriors’ jijini Dar es Salaam kwenye mechi ya mchujo ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani Gabon na Guinea ya Ikweta.