Na. Johary Kachwamba – MAELEZO, DODOMA
JAMII imetakiwa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi nchini katika kutoa taarifa zitakazo fanikisha kukamatwa kwa wote walioshiriki mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Pereira Silima bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Al -Shaimaa Kwegyir, Mbunge wa Viti Maalum aliyehoji kuchelewa kwa taarifa ya kupatikana kwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Pendo Emmanuel.
“Pendo alitekwa kutoka mikononi mwa mama yake mzazi, hii changamoto ni kubwa sana, tunaomba jamii itusaidie kutoa taarifa zitakazo saidia kufanikisha kukamatwa kwa wahusika, tushirikiane kwa pamoja kukomesha tatizo hili” alisema Mhe. Silima
“tangu kutekwa kwa mtoto Pendo watu 14 wanashikiliwa na jeshi la polisi akiwemo baba mzazi, uchunguzi bado unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani hivi karibuni, ila Pendo bado hajapatikana” aliongezea Mhe. Silima
Aidha akijibu Swali la msingi la Mhe. Salumu Barwany, Mbunge wa Lindi Mjini, aliyehoji idadi ya kesi za mauaji ya walemavu wa ngozi na sababu za kuchelewa kutolewa hukumu. Mhe. Silima alisema kesi 10 zinaendelea kisikilizwa mahakama mbalimbali
“kati ya mwaka 2006 hadi 2015 jumla ya matukio 56 ya uhalifu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa nchini. Matukio 41 yalihusisha vifo 43, matukio 13 yalihusisha majeruhi 13 na matukio 2 ya kupotea kwa watu wenye ulemavu wa ngozi” alifafanua Mhe. Silima
“kesi 46 kati ya matukio 56 zilifikishwa Mahakamani ambapo kesi 10 zenye watuhumiwa 12 zilitolewa hukumu ya kifo na kumi ziko chini ya upelelezi. Aidha kesi 26 watuhumiwa wake waliachiwa huru kwa kukosa ushahidi” aliongezea Mhe. Silima
Kuchelewa kwa hukumu au upelelezi wa baadhi ya kesi zilizotajwa kunachangiwa na sababu mbalimbali kama vile matokeo ya uchunguzi wa DNA toka Mamlaka ya Uchunguzi na/au mashahidi kutopatikana kwa urahisi na kwa wakati.