JAMBO LEO YAIVUA GAMBA UHURU

Kikosi cha timu ya Jambo Leo

TIMU ya soka ya Jambo Leo ‘Wagumu Star’ jana imeibanjua timu ya soka ya Uhuru inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ‘wazee wa kujivua gamba’ katika mashindano ya Kombe la NSSF yanayoendelea jijini Dar es Salaam kwa kushirikisha vyombo vyote vya habari.

Katika mchezo huo ulofanyika jana kwenye uwanja wa Sigara (TTC) Chang’ombe, Jambo Leo imeifunga Uhuru 1-0 matokeo ambayo timu ya Uhuru imeonekana kushukuru kwa kufungwa bao moja tofauti na walivyotegemea.

Timu ya Jambo Leo ambayo imekuwa ikigawa dozi ya mabao matatu mpaka manne kwa kila timu ambayo inakutana nayo, katika mashindano hayo kiasi cha kuogopwa na kila timu.

Uhuru walionekana kucheza mchezo wa kujiami tangu mwanzo kwani wachezaji wake hasa golikipa alionekana kuchelewesha mipira mithiri timu yake imeshinda jambo ambalo liliwafanya vijana wa Jambo Leo kupunguza kasi kadri ya muda ulivyokuwa ukiyoyoma.

Hadi mapumziko Uhuru ilikuwa ikicheza kwa kujiami huku wakitarajia kumalizika kwa pambano hilo wakiwa sare ili wakabahatishe kwenye penati katika mchezo huo wa nusu fainali.

Kipindi cha pili vijana wa Jambo Leo waliishtukia janja ya wapinzani wao na kuanza kuongeza kasi ya mchezo na kuwachanganya kabisa vijana wa Uhuru na katika dakika ya 72 walijipatia goli la shuti kali lililomshinda mlindamlango wa Uhuru na kukubali yaishe.

Hadi mpira unamalizika Jambo Leo ilikuwa na goli moja huku Uhuru wakiambulia patupu. Jambo Leo haijapoteza mchezo hata mmoja tangu kuanza kwa mashindano hayo hadi imeingia fainali. Hata hivyo Uhuru walionekana kuridhika na matokeo hayo kwani walijua katika mchezo huo wangeliangushiwa mvua ya magoli kama ilivyokuwa kwa kila timu inayokutana na Jambo Leo.

“Tunashukuru mungu sisi tumefungwa goli moja wenzetu wamekuwa wakifungwa 3, 4, hadi 7, hivyo tumejitahidi kwa matokeo haya…tumewabana kweli kweli,” alisema mmoja wa wachezaji wa timu ya Uhuru alipozungumza na HM. Mashindano hayo yanaendeleoa tena leo.