Jambazi laua askari kwa risasi Arusha

wa Jeshi la Polisi Mkoa Arusha, Thobias Andengenye

*Lamjeruhi pia Mkuu wa Upelelezi

Na Mwandishi Wetu, Arusha

KONSTEBO wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha namba F 2218, wa Idara ya Upelelezi, Kijanda Mwandu amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na jambazi. Wakati jambazi hilo likimuua askari huyo pia limemjeruhi kwa risasi Mraribu Msaidizi wa Polisi, ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arusha, Faustine Mafwele .

Akizungumza jana mjini Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa hapa, Thobias Andengenye amesema tukio hilo limetokea Januari 3 mwaka huu majira ya saa 10 alfajiri eneo la Shangarai wilayani Arumeru. Andengenya alisema siku ya tukio askari walikuwa doria wakifuatilia taarifa za kuwapo kwa jambazi katika eneo hilo la barabara mpya ya Peace Point.

Kamanda Andengenye aliongeza kuwa polisi hao walipofika katika nyumba aliyokuwa jambazi huyo, ghafla alianza kuwashambulia kwa bunduki aina ya SMG. Amesema marehemu alipigwa risasi shingoni na kufariki papo hapo na risasi nyingine kumjeruhi OC CID katika bega la kushoto, ambapo kwa hivi sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Selina Lutheran ya mjini hapa.

Aidha Kamanda Andengenye alimtaja jambazi huyo kuwa ni Pokea Henry au Samson Kaunda ambaye alifanikiwa kutoroka baada ya kufanya tukio hilo. Alisema kuwa nyumba hiyo aliyokuwamo jambazi huyo inamilikiwa na Agness Silas ambaye naye alitoroka na jambazi huyo baada ya tukio hilo huku akidaiwa kupiga risasi zaidi ya 15 kwa lengo la kuwashambulia polisi.

Andengenye alisema kuwa upekuzi ulipofanyika ndani ya nyumba hiyo asubuhi, polisi walikuta risasi 36 za SMG, risasi 12 za Shortgun, kitako 1 cha shortgun, mtambo wa bunduki ukiwa umefunguliwa pamoja na soksi 2 za kuvaa usoni zinazotumiwa na majambazi hao.

Alisema kuwa polisi hao walipokuwa wakiendelea na upekuzi katika kijiji cha jirani na eneo hilo cha Nambala, walifanikiwa kukuta bunduki aina ya SMG iliyokuwa na risasi 19 ambayo ilikuwa imetumbukizwa katika shimo la choo.

Alidai kuwa katika kijiji hicho mwanamke aliyefahamaika kwa jinala la Rehema Ally ambaye anadaiwa kuhifadhi majambazi nyumbani kwake, ndipo bunduki hiyo inadhaniwa kutupwa na mmoja wa washiriki wa Elipokea ilipatikana.

Aliongeza kuwa Disemba 27 mwaka huu walimkamata Rehema aliyekuwa akitafutwa na polisi baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa ‘anafuga’ majambazi nyumbani kwake. Kufuatia tukio hilo jeshi hilo linamshikilia Rehema, pamoja na Daines Msawe (9) na Alex Parumina (13) ambaye anadaiwa kumfungulia mlango jambazi kabla ya kuanza kuwashambulia polisi.

Alisema watoto hao walikutwa nyumbani kwa Agness na wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi juu ya tukio hilo wakati jeshi hilo likiendelea na operesheni ya kumsaka jambazi hiyo ambaye awali anadaiwa kuwa alifungwa magereza pamoja na Agness. SACP Andengenye alisema kuwa donge nono la milioni 5 litatolewa kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa jambazi huyo na wenzake.