RAIS mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametoa msameha kwa wanachama wote wa shirikisho hilo waliofungiwa chini ya Utawala wa rais aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga, isipokuwa tu wale ambao adhabu zao zinatokana na makosa ya rushwa na kupanga matokeo.
Maana yake- Michael Richard Wambura aliyekwama kabisa kugombea nafasi yoyote chini ya utawala wa Tenga, sasa yuko huru kugombea au kuteuliwa kwa nafasi yoyote ya uongozi katika soka ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi uliomalizika usiku wa manane jana ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam, Malinzi aliiagiza Sekretarieti ya TFF chini ya Katibu wake, Angetile Osiah mara moja kuandika barua za misamaha kwa wote wanaotumikia adhabu za utawala wa Tenga.
“Hata rais wa nchi anapoingia madarakani huwa anatoa misamaha, nami nachukua fursa hii kuomba ridhaa yenu Wajumbe, kwa kuwa huu ni uongozi mpya, basi tufungue ukurasa mpya, nipeni ridhaa yenu, watu wote waliofungiwa chini ya utawala uliomaliza muda wake, wasamehewe tuanze upya. Isipokuwa wale tu ambao adhabu zao zinatokana na rushwa na upangaji matokeo,” alisema Malinzi.
Malinzi alisema muda si mrefu atakutana na Kamati yake ya Utendaji kujipanga na amewataka wajumbe wote kujiandaa kwa hilo. Kwa upande wake, Tenga pamoja na kumpongeza Malinzi, aliahidi kumkabidhi ofisi Jumamosi ijayo. Malinzi ameshinda Urais wa TFF baada ya kupata kura 72, dhidi ya 52 za mpinzani wake Athumani Jumanne Nyamlani.
Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam, Walace Karia alifanikiwa kushinda nafasi ya Makamu wa Rais kwa kupata kura 67 akiwashinda Nassib Ramadhani kura 52 na Imani Madega sita.
Katika nafasi za Ujumbe; Kanda ya 13; kiungo wa zamani wa Simba SC Wilfred Kidau amepata kura 60 na kuwashinda Muhsin Said kura 50, Omar Abdulkadir kura 10 na Alex Kabuzelia kura nne. Kanda 12; Khalid Mohamed Abdallah amepata kura 69 na kumshinda Davisa Mosha aliyepata kura 54.
Kanda ya 11 Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amepata kura 78 na kuwashinda Riziki Majala kura tano, Twahir Njoki kura mbili, Juma Pinto kura 26 na Farid Mbaraka kura 14, Kanda ya 10 ameshinda Hussein Mwamba aliyepata kura 63, huku Charles Komba akipata nne na Stewart Nasima 58.
Kanda ya tisa Othman Kambi aliyepata kura 84 yeye amewashinda Francis Bulame kura 30, wakati James Mhagama aliyepata 93 amemshinda Zafarani Damoda aliyepata kura 11 na Kanda ya nane, Ngube Kiondo aliyepata kura 73 amemshinda Ayoub Nyaulingo kura 52.
Kanda ya Tano, Ahmed Iddi Mgoyi aliyepata kura 92 amemshinda Yussuf Kitumbo aliyepata kura 34, wakati Omar Walii Ali ameshinda Kanda ya nne kwa kura 53 dhidi ya 19 za Ally Mtumwa.
Eley Mbise ameshinda Kanda ya Tatu kwa kura 51 dhidi ya 53 kura 57 za Lamanda Swai.
Mbasha Matutu aliyepata kura 63, amembwaga Vesastis Ligano aliyepata kura 61 katika Kanda ya Pili, wakati Vedastus Lufano aliyepata kura 51, amewashinda Jumbe Odesa Magati kura 11, Mugisha Galibona kura 24 na Samuel Nyalla kura 39 katika kanda ya saba na Kanda namba moja, Karilo Samson hakuwa na mpizani akapita moja kwa moja.
CHANZO: Bongostaz blog