Jaji Warioba ataka vyama vya siasa vijifunze kushindana

Jaji Joseph Warioba

*Asema kila awamu ilikuwa na matatizo yake

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema vyama vya siasa nchini havina budi kujifunza kushindanisha sera na kuimarisha demokrasia ndani ya vyama vyenyewe.

Amesema hayo Jumanne, ya Oktoba 11, 2011 mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Swali aliloulizwa lililenga kufahamu Jaji Warioba kama mmoja wa viongozi waliofanya kazi karibu sana na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anatoa wito gani kwa Watanzania kuhusu masuala ambayo hayati Baba wa Taifa alikuwa akiyasimamia.

Alisema kulikuwa na mambo mengi lakini kubwa ni umoja na amani ambayo ndiyo ilikuwa misingi mikubwa ya Taifa hili na kwamba hata katika mfumo wa vyama vingi bado kuna haja ya kuendeleza utulivu na amani vilivyokuwepo.

Alisema vyama vya siasa havina budi havina budi kujifunza kushindanisha sera ili wananchi waweze kuchagua chama ambacho wanaona sera zake zinafaa na siyo kushindana kwa maneno tu.

“Sasa hivi ukitazama magazeti ya kila siku, sote tunazungumzia siasa tupu…ni lazima tutambue kuwa tukimaliza uchaguzi, tunaingia katika shughuli za kuleta maendeleo, tujiepushe na kampeni za uchaguzi zisizoisha,” aliongeza.

Alisema vyama vya siasa havina budi pia kuhakikisha kuwa vinaimarisha demokrasia nchini na ndani ya vyama vyenyewe na kuongeza kwamba: “Demokrasia ni pamoja kutofautiana mawazo bila kupigana.”

Alisema kama kuna suala linaisumbua nchi, kuna haja ya kukaa pamoja na kutafuta njia mbadala kwa maslahi ya Taifa. “Sisi na kundi jingine hatuna budi tukae pamoja na kujiuliza ni nini cha kufanya ili tusonge mbele… na hapa nataka kusisitiza kuwa kila awamu ilikuwa na matatizo yake, hakuna wakati ambapo nchi yetu haikuwa na matatizo lakini tulikaa pamoja na kutafuta ufumbuzi,” alisema.

Akifafanua zaidi, Jaji Warioba alisema katika awamu ya kwanza kulikuwa na uasi wa jeshi, vita vya kumng’oa nduli Iddi Amin, kulikuwa na msukosuko wa kiuchumi baada ya kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika Mashariki lakini yote yalitatuliwa na nchi ikasonga mbele.

“Mimi nilipoingia madarakani (1985-1990) wakati awamu ya pili chini ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, nchi haikuwa na bidhaa madukani kwa sababu tulikuwa hatuna fedha za kigeni za kutosha kuagiza bidhaa nje ya nchi; nchi ilikumbwa na baa la njaa lakini tulimaliza tatizo la njaa, tukazalisha kwa wingi zaidi mpaka ikabidi tuanze kujenga maghala kwa ajili ya kuhifadhi chakula cha ziada,” alisema.

“Tulitumia umoja wa nchi yetu kutatua matatizo yaliyoikumba nchi na mara tatizo lilipotokea hatukunyoosha kidole kwa mtu mmoja… lilikuwa ni tatizo la wote.”

Alisisitiza haja ya kuilinda misingi ya umoja wa kitaifa na kutambua juhudi za kuleta maendeleo lakini akaongeza kuwa kuwa kuna haja ya kuangalia changamoto zinazojitokeza na kuainisha njia za kukabiliana nazo.