Jaji Ramadhani Aitaka Afrika Kuzingati Haki za Binadamu

Jaji Augustino Ramadhani

Jaji Augustino Ramadhani


Na Mtuwa Salira, EANA-Arusha

RAIS wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), Jaji Augustino Ramadhani amezitaka nchi za Afrika kuzingatia zaidi masuala ya haki za binadamu kama kweli zinataka kupiga hatua za kiuchumi na kidemokrasia.

Akifungua semina ya kuhamasisha mataifa ya Afrika kuiunga mkono mahakama hiyo mjini Addis Ababa, Ethiopia mwishoni mwa wiki, Jaji Ramadhani alisema kwamba matarajio ya kufanikiwa kwa Agenda ya Afrika ya 2063 yanategemea sana umuhimu unaotolewa katika masuala ya uhamasishaji, ulinzi na kunufaika na haki za binadamu na watu barani Afrika.

“Historia inatufundisha kwamba kuheshimu haki za binadamu, kuhamasisha maendeleo ya binadamu na kuimarisha amani pamoja na nia njema ya kuleta maendeleo ya kisiasa na kiuchumi ni mambo ya msingi ya kuzingatia ili kujipatia maendeleo ya maana,” aliwaambia wajumbe zaidi ya 100 wakiwemo kutoka serikali, balozi za Kiafrika, wanasheria, wanafunzi, mashirika yasiyo ya kiserikali, waandishi wa habari na wanaharakati.

Kwa mujibu wa taarifa ya AfCHPR ambayo nakala yake ilitolewa kwa Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) Rais wa mahakama hiyo alitoa changamoto kwa nchi za Afrika kuiunga mkono mahakama yake yenye makao yake makuu mjini Arusha, Tanzania, ambayo ndiyo mahakama pekee ya Umoja wa Afrika (AU).

“Umuhimu wa uwepo wa mahakama hiyo unategemea kuungwa mkono na wadau hususan ni nchi wanachama wa AU,” alisema Jaji Ramadhani ambaye pia ni Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania.

Alikumbusha kwamba tangu kupitishwa kwa itifaki ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo mwaka 1998 ni nchi 28 tu kati ya 54 wanachama wa AU ndiyo zilizoridhia mkataba wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo na kuongeza kwamba kati ya hizo, ni nchi saba tu ndizo zilizopitisha azimio la kuruhusu watu binafsi na mashiriki yasiyo ya kiserikali kufikisha kesi moja kwa moja kwenye mahakama hiyo. Alizitaja nchi zilizotoa ruhusa hiyo kuwa ni pamoja na Tanzania,Burkina Faso, Ivory Coast, Ghana, Malawi, Mali na Rwanda.

Naye katika hotuba yake ya ufunguzi, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Ethiopia, Reta Alemu Nega alisema sasa Afrika inajisimamia yenyewe kwa kubeba majukumu yake ya kuhamasisha na kulinda haki za binadamu.