Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi amezitaka Redio za Jamii kutokubali kutumiwa na vyama vya siasa vinavyotumia unyonge wa watanzania kiuchumi kujinufaisha kisiasa.
Alisema kwa kufanya maamuzi ya kutotumiwa na vyama vya siasa kutasaidia kuepusha migogoro inayochochewa na taarifa za kishabiki za vyamja vya siasa.
Jaji Mutungi alisema hayo wakati akichangia mada tatu zinazohusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi 2010, Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya vyama vya Siasa zilizotolewa kwa viongozi na wamiliki wa redio jamii nchini katika warsha inayoendelea mjini hapa.
Aliwataka washiriki wa warsha hiyo ya siku nne inayohusu utekelezaji wa mradi wa kuendeleza majadiliano kwa njia ya amani kwa lengo la kukuza demokrasia nchini, kutambua kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia unyonge wa kielimu na uchumi wa watanzania kuwaahidi mambo yasiyotekelezeka jambo ambalo amesema ni matumizi mabaya ya uhuru wa taasisi.
Alisema vyombo vya habari vya jamii bado visafi na vina nafasi kubwa kubadilisha mitazamo ya utamaduni wa siasa chafu iliyojengeka kuwa maendeleo ni kupata uongozi wa siasa, tena kwa kauli za uwongo na kujenga chuki.
“Maendeleo ni kuchagua kiongozi ambaye ni mwadilifu, mwenye uchungu na taifa na yuko tayari kuitunza amani tuliyoirithi baada ya kupata uhuru wa nchi.” alisema Jaji Mutungi.
Mada hizo ziliwasilishwa na Wasaidizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa Ibrahim Sapi Mkwawa, Sisty Leonard Nyahoza na Ofisa Sheria Mwandamizi Piencia Etanga kutoka ofisi ya Msajili wa Vyama Vingi vya Siasa.
Msajili wa Vyama Vingi amesema, kwa kuwa Redio Jamii ndiyo zinazowafikia watanzania wenye maisha ya kawaida walio wengi vijijini na ndio wanaofuatwa na wanasiasa wa namna hiyo ili wawaunge mkono nia zao bila kujali maslahi ya wananchi.
Amezitaka redio jamii kuunganisha nguvu ya pamoja na wadau wakuu wa mradi wa uchaguzi kwa kuwaelimisha wananchi, kusema ukweli bila woga kitu chenye manufaa kwa umma hasa kuhusu wanasiasa matajiri kutumia raslimali zao katika kutafuta kura hali ambayo imeliingiza taifa katika wimbi la rushwa na umaskini wa kupindukia. Alisisitiza kuwa siasa ni ushindani na kushinda hivyo zisirubuniwe kirahisi kwa pesa ambazo sio msingi wa maendeleo.
“Pesa sio msingi wa maendeleo, msikubali kurubuniwa wala kununuliwa na wachache wanaotumia nguvu ya pesa. Silaha kubwa ni kuunganisha nguvu na vyombo vya habari jamii tutafanikiwa kulijenga taifa.”
Wakati huo huo ofisi ya Msajili wa Vyama Vingi imekuwa ikikabiliwa na matatizo kutokana na udhaifu wa sheria ambao wanasiasa wamekuwa wakiutumia kwa kutoa lugha chafu na za uchochezi ili waweze kuungwa mkono bila kujali maslahi ya taifa.
Mada nyingine iliyotolewa katika mkutano huo wa siku nne uliofadhiliwa kwa ushirikiano wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNDP na UNESCO iliyofanyika katika Ukumbi wa Waziri Mkuu mjini Dodoma ni Jinsia na Kuhusisha Makundi Maalum Katika Uchaguzi 2015 na Margareth Rugambwa kutoka Shirika la Umoja wa Kimataifa linaloshughulikia Kuwapatia Uwezo Wanawake (UN Women).
Katika semina hiyo washiriki wameazimia kutumia redio jamii katika kufanikisha mawasiliano baina ya wananchi na vyombo vinavyosimamia masuala ya uchaguzi na siasa.