Jaji Mark Bomani Ashauri Kura za Maoni Kuamua Muundo wa Serikali

Jaji Mark Bomani

Na Belinda Kweka – MAELEZO, DSJ

MWANASHERIA Mkuu wa Kwanza mstaafu wa Serikali, Jaji Mark Bomani ametoa wito wa kupingwa kura ya maoni kwa wakazi wa Tanzania Visiwani ili kuona kama wanahitaji mfumo gani wa muungano kabla ya kuendelea na mchakato wa sasa wa rasimu ya Katiba mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Jaji Bomani alisema anaipongeza tume ya Jaji Joseph Warioba kwa kazi nzuri na pia kwa mapendekezo yake juu ya Muungano wa Tanzania.

Kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo Jaji Bomani alitoa historia fupi juu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo ameeleza kuwa muungano huo ulipendekezwa na hayati Sheikh Abeid Amani Karume na hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambao walikutana mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari, mwaka 1964.

Jaji Bomani aliongeza hayati Karume alipendelea nchi mbili kuungana na kuwa nchi moja, lakini hayati Nyerere alisita kidogo kwa kuogopa kwamba ingeonekana Zanzibar imemezwa na Tanganyika na pengine kuleta maasi Zanzibar hivyo kupendekeza kuundwa mfumo wa muda mfupi wakati mfumo wa kudumu ukifanyiwa kazi.

“Suala la Muungano ndilo suala kubwa kuliko yote katika mchakato wa Katiba mpya. Niliwahi kuto ushauri nao ni kwamba ifanyike kura ya maoni ya wananchi hasa Zanzibar kama wanautaka muungano au la na kama wanautaka uwe muungano wa mfumo gani? Mpaka sasa maoni ambayo yanasikika ni maoni ya viongozi mara Zanzibar ijitoe kwenye muungano mara tuwe na muungano wa mkataba,” alisema Jaji Bomani.

Akijibu maswali aliyoulizwa na waandishi wa habari, Jaji Bomani amesema katika uundwaji wa Serikali tatu anaamini utaweza kumaliza migogoro inayojitokeza mara kwa mara hasa upande wa Zanzibar kuogopa kumezwa.

“Woga wa gharama za mfumo wa Serikali tatu hauna msingi. Inategemea Serikali hizo unazifanya vipi, ipo mifano mingi mno duniani ya miungano ya mfumo mbalimbali,” alisisitiza.

Pia ameongezea kuwa kama kutaundwa Serikali tatu basi iwe Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Akiongezea kuhusu katiba mpya amesema “kwa maoni yangu si lazima kazi hii ya katiba iishe kabla ya 2015, tupate muda wa kutosha ili tuweze kupata katiba ya kueleweka na kukubalika na kila mtu,”.