JAJI CHANDE AHIMIZA MABADILIKO KATIKA MAHAKAMA ZA AFRIKA MASHARIKI

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande amezitaka mahakama katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wake wa utendaji ili kuleta ufanisi na maamuzi ya haki kwa wakati kwa wananchi wa kanda hiyo.
Alisema hatua hiyo itarejesha imani na matumaini kwa mahakama katika nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kuacha ugoigoi katika kushughulikia mabadiliko ndani ya mahakama na utoaji huduma kwa masuala ya uchumi na fedha katika mwenendo mzima wa mtangamano.
‘’Tusiruhusu mabadiliko katika mahakama yabaki kama vile agenda isiyo na mpango. Hii ni changamoto kubwa,’’ alisema Jaji Chande alipokuwa anafungua mkutano wa Tatu wa Majaji Wakuu wan chi za Afrika Mashariki mjini Dar es laam, Aprili 16.
Jaji Mkuu huyo wa Tanzania, alisema huduma zilizokuwa zinatolewa na mahakama zote katika nchi wananchama wa EAC ni chini ya kile kilichokuwa kinatarajiwa kufanywa kwa jamii yenye kuendelea kuwa na uelewa mkubwa.
‘’Moja ya kizibiti cha kuonyesha jamii imekata tamaa na utendaji wa mahakama ni pamoja utendaji wa chini ya kiwango wa vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria na kujichukulia sheria mkononi,’’ alisema na kusisitiza kwamba juhudi hazina budi kufanywa ili kuhakikisha kwamba upo utawala wa sheria kuonyesha uwepo wa mahakama, kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Sekretarieti ya EAC.
Alitoa changamoto kwa wanasheria kuzifahamu fika sheria za EAC ikiwa ni pamoja na ngazi mbalimbali za mtangamano wa EAC.
‘’Ni wanasheria wetu wangapi ambao tunaweza kusema wanazifahamu sheria za Jumuiya?,’’ aliuliza majaji,mahakimu na maafisa wengine wa mahakama waliokuwa wanamsikiliza kwa makini kutoka nchi wanachama na Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ).
Naibu Katibu Mkuu wa EAC, anayeshghulikia Shirikisho la Kisiasa, Beatrice Kiraso, alisema kuziwezesha idara za mahakama za kanda kushughulikia masuala ya mtangamano ni muhimu hususan ni wakati huu ambapo kutokuwapo uhuru wa masuala yote yanayohusiana na uzalishaji.
Aliipongeza EACJ ambayo pamoja na changamoto nyingi inazokabiliana nazo, imechukua hatua ya kutafsiri mambo mbalimbali yanayohusiana na Mkataba wa EAC.