Jaji Bomani afungua mkutano wa Wahariri Arusha, awataka kulinda maadili ya taaluma

Jaji Mark Bomani (aliyesimama), akiwahutubia wahariri wa habari jana mjini Arusha kabla ya kufungua mkutano huo rasmi. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini na wa kwanza kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya SBL, Teddy Mapunda pamoja na Katibu wa Jukwaa la Wahariri Bonifas Meena

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Serengeti Breweriers (SBL), Jaji Marck Bomani, amewataka wahariri wa habari nchini kutokubali kufanya kazi yao kwa shinikizo la watu na kutelekeza maadili ya taaluma hiyo.

Amesema vyombo vya habari ni muhimu kutokana na kazi yao kubwa kwa jamii hivyo ni vema vikafanya kazi kwa kufuata maadili ili visije vikaupotosha umma unaofitegemea kwa elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali.

Jaji Bomani alitoa changamoto hiyo jana mjini Arusha alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa vyombo vya habari kutumia lugha nyepesi ityakaoeleweka kirahisi na jamii nzima wanapofanya kazi zao ili kutoa haki kwa Wananchi wote. Alisema upo mtindo wa baadhi ya vyombo vya habari kutumia lugha ngumu ambayo imekuwa ikiwaacha njia panda wasomaji wachache jambo ambalo si zuri kufanywa na muhimili wa habari ambao unategemewa na jamii yote.

Katika mkutano huo ambao umedhaminiwa na kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Jaji Bomani pia aliwataka waandishi wa habari kuhakikisha wanaendelea kuwa na elimu za taaluma nyingine mbali ya masuala ya habari ili waweze kuchambua mambo kwa kina na lugha rahisi.

“Wakati mwingine ni vizuri mwandishi wa habari za biashara akasome pia masuala ya fani hiyo kama uchumi, hii itamsaidia anapoandika na kufanya uchambuzi wa masuala hayo…atachambua kwa kina pia hawezi kupotosha,” alisema Bomani ambaye pia ni Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Aliongeza kuwa kusomea taaluma nyingine zinamjenga mwanahabari kuwa na uelewa mpana wa masuala anuai hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kutambua kwa haraka hata sehemu ambayo anadanganywa na mtoa taarifa kuhusiana na suala fulani.

“Kwa mfano unapomuandia Mtanzania wa kawaida kwamba uchumi mwaka huu umekuwa kwa asilimia kadhaa ukilinganisha na mwaka jana, hakuelewi kwani yeye haoni mabadiliko yoyote…sasa nijukumu lenu kumchambulia mambo hayo kwa lugha rahisi,” alisema Jaji Bomani.

Mkutano huo unaendelea leo ambapo mada mbalimbali zitatolewa kwa wahariri na kuzijadili kwa kina kabla ya kutoka na msimamo mmoja kuhusiana na changamoto anuai ndani ya tasnia ya habari Tanzania.


Baadhi ya wahariri wakiwa mkutanoni