Jaji ajitoa kesi ya mbunge Lema

Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande

Na Janeth Mushi, Arusha

JAJI Aloyce Mujulizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha aliyekuwa akisikiliza kesi ya kupinga matokeo inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) amejitoa kusikiliza kesi hiyo.

Jaji Mujuni amefikia hatua hiyo leo mjini hapa, huku akisisitiza kuwa Mbunge Lema lazima awasilishe ushahidi wake wa kutaka jaji huyo kujitoa katika shauri hilo, ambapo amempa siku tano. “Ninalazimika kumwamrisha Lema kuhakikisha anakamilisha ushahidi wake na kuuwasilisha mahakamani na kunipatia nakala yake kwa siku
zisizozidi tano,” alisema Jaji.

Leo kesi hiyo ingeendelea ambapo upande wa wadai ulitakiwa kutoa ushahidi jambo ambalo halikufanyika zaidi ya Mahakama kusikiliza pingamizi zilizowasilishwa na Wakili, Alute Mungwai kupinga maombi ya Wakili wa Lema, Method Kimomogolo.

Kimomogolo aliwasilisha maombi mahakamani hapo ya kumtaka Jaji huyo kujiengua kusikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa Jaji huyo alipokuwa wakili katika kampuni ya Ima Advocates, kampuni hiyo ilituhumiwa na CHADEMA kwa madai ya kukwapua mabilioni Benki Kuu (BOT) ya EPA.

Awali Oktoba 28 mwaka jana shauri hilo lilikwama kuendelea kusikilizwa baada ya wakili Kimomogolo kutoa maombi kwa mahakama kuwa Jaji ajitoe kwenye shauri hilo kwa madai ya Lema, Aloyce Mujulizi na wafuasi wao kutokuwa na imani na Jaji, kufuati maneno yaliyonukuliwa katika gazeti la Nipashe yaliyodaiwa kutolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.

Nape alidaiwa kusema kuwa wanan uhakika wa kushinda katika kesi
hiyo, hivyo Chadema wana uhakika kuwa Jaji amewathibitishia CCM ushindi huo, ambapo mahakama ilichunguza madai hayo na kuonekana kuwa Nape alinukuliwa vibaya. Jaji Mujulizi alipokuwa akiahirisha shauri hilo Novemba 16 mwaka jana alimtaka Kimomogolo, kupima kama bado hawana imani na Jaji huyo.

“Imeonyesha dhahiri kuwa bado hawana imani na jaji kutoa uamuzi kwani wameniletea taarifa kuwa wanakusudia kuleta hoja hiyo kwa kutoa vigongo vizito zaidi kwa siwezi kutenda haki, hivyo CHADEMA kimetoa taarifa rasmi,” alisema Jaji.

Jaji Mujulizi aliieleza mahakama hiyo kuwa CHADEMA kimemtuhumu kwa
madai ya kuwa Kapuni ya uwakili aliyokuwa anafanyia kazi kabla ya kuwa Jaji kuwa waliiba fedha na kukisadia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wake Mkuu wa mwaka 2005.

Kufuati madai hayo Jaji huyo alimweleza Kimomogolo kuwa, anachokijua ni kwa CHADEMA kwa kipindi cha mwaka 2006/07 imekuwa ikiituhumu kampuni yake kwa kuisajili kampuni ya Deep Green na siyo kuchukua fedha toka BOT kwenda.

Jaji alimuhoji Kimomogolo kwa zaidi ya mara mbili iwapo ana uhakika na madai ya kuwa kampuni hiyo ya uwakili ilituhumiwa kwa kuhusika na
ukwapuaji huo wa fedha, ambapo wakili huyo alijibu ana uhakika kwa
mujibu wa maelezo ya CHADEMA.

“kwa heshima ya kutenda haki kwa shauri hilo najitoa ili jamii
inayofuatilia shauri hilo isipoteze imani na mimi kwa madai ya kuwa
sitaweza kusikiliza na kutoa maamuzi ya kesi hii,” alisema Jaji

Jaji huyo liwataka Lema, Kimomogolo pamoja na CHADEMA kuchukua hatua za kikatiba kwa kuwasilisha rasmi maombi kwa Rais, kuunda tume ya kuchuinguza jambo hilo na kuliweka wazi.