Jairo asimamisha kazi rasmi, ni juu ya tuhuma zinazomkabili


David Jairo

Dodoma

KATIBU Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo amemsimamisha kazi Katibu wa Nishati na Madini, David Jairo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za kuchangiza zaidi ya sh. bilioni moja kinyemela.

Jairo anaanza kutumikia adhabu hiyo leo, huku akimpisha Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa fedha zinazodaiwa kuchangishwa na Katibu Mkuu huyo ili kuwashawishi wabunge waipitishe bajeti ya wizara yao.

Akitoa taarifa hiyo jana mjini hapa kwa waandishi wa habari, Luhanjo alisema; CAG atafanya ukaguzi kwa siku 10 kulingana na sakata lenyewe lilivyo. Luhanjo alisema hatua hiyo iliyochukuliwa dhidi ya, Jairo ni kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002.

“Nimeona niwaambie hili, ili tusiendelee kuwaambia tunamsubiri Rais wakati, mimi mwenye kusimamia nidhamu nipo hapa, hii ni hatua mojawapo ambayo nimeichukua.

Hizi ni tuhuma ni nzito sana, ndio tumeamua aende likizo yenye malipo kupisha uchunguzi. Kwa mamlaka niliyo nayo, nimeamuru uchunguzi huo ufanyike kwa lengo la kupata ukweli kuhusu tuhuma.

Kama mnavyofahamu, mnamo Julai 18 mwaka huu, wakati wa majadiliano ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, baadhi ya wabunge, wakati wakichangia hotuba hiyo walimtuhumu, Jairo kuhusika na tuhuma za kuzitaka Taasisi na Idara zilizo chini ya Wizara hiyo zichangie kila moja sh. milioni 50, 000, 000 kwa ajili ya kuwezesha bajeti ya wizara hiyo iweze kupita,” alisema Luhanjo.

Katibu Mkuu huyo Kiongozi alisema tuhuma nyingine ni kwamba zilipangwa kuwalipa wabunge ili kufanikisha mawasilisho ya bajeti ya wizara, na kuwalipa masurufu ya safari watumishi walio chini ya Wizara na Taasisi zake ambao tayari walishalipwa na wizara na taasisi zao.

Alisema baada ya uchunguzi wa awali zipo hatua ambazo zitafuata, ambapo alisema kuwa hatua hizo zitategemea matokeo ya uchunguzi huo wa awali ambapo kama atakutwa na hatia atapewa Hati ya Mashitaka kama itakavyokuwa imependekezwa na CAG.

“Lengo la kufanya uchunguzi huo ni kutaka kumpa fursa ya kujitetea kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma. Kama mnavyojua, Katibu Mkuu alituhumiwa na wabunge, na yeye hana nafasi ya kujitetea ndani ya ukumbi wa Bunge, na ni lazima tuhuma zipate maelezo ya upande wa pili, na hapa ndipo sheria hii ya Utumishi wa Umma inachukua nafasi yake,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana alibanwa bungeni kwa kushindwa kumwajibisha, Jairo anayetuhumiwa kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Akiuliza swali la papo kwa papo, Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF), alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais ana mamlaka ya kufanya kazi za rais endapo hayupo.

Na kuhoji kuwa “Je, Waziri Mkuu haoni kama amevunja Katiba uliposema tumsubiri rais aje kutoa uamuzi juu ya suala la Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini. Huoni kama umekwenda kinyume na katiba hiyo kwasababu Makamu wa Rais yupo? alihoji Abdallah.

Pinda akijibu swali hilo alikiri kupewa wakati mgumu na mbunge huyo na kusema kuwa “Mheshimiwa mbunge umenipa mtihani ambao sikuutegemea.

“Ni kweli Makamu wa Rais ana mamlaka ya kuongoza nchi wakati rais hayupo nchini, na kama na makamu hayupo basi hata Waziri Mkuu anamamlaka hayo.

Lakini kwa mujibu wa Katiba hiyo hiyo kwamba iwapo tumeachiwa madaraka ya kuongoza nchi wakati raisi hayupo si kila kitu tunaweza kufanya.

Hivyo isingekuwa rahisi kwa Makamu wa Rais kuanza kusema sasa nimeukata nakufukuza, hapana sisi tuna ukomo, hatuwezi kutoa msamaha wa kusamehe wafungwa, hivyo lazima Rais ashirikishwe kwanza ili kuondoa dhana kwa nchi haina kiongozi wake,” alisema Pinda.