Italy kuwekeza zaidi kwenye sekta ya utalii

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba Ikulu, Zanzibar

ITALY imeeleza azma yake ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya utalii na sekta nyenginezo hapa nchini na kupongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.

Hayo yalielezwa na Balozi wa Italy nchini Tanzania Mhe. Peirliugi Velardi alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Balozi Verladi alisema kuwa Italy imeamua kwa makusudi kuzidisha miradi ya uwekezaji nchini Tanzania ikiwemo Zanzibar ambapo tayari nchi hiyo imeshaweka mikakati maalum juu ya sekta hiyo hapa nchini.

Alisema kuwa Italy imekuwa na uhusiano na ushirikiano mwema na Zanzibar hatua ambayo imesaidia kuimarisha na kuendeleza sekta ya Utalii hapa Zanzibar.

Balozi huyo alisema kuwa mbali ya sekta ya Utalii nchi yake hivi sasa ina mpango wa kuimarisha uwekezaji katika sekta mbali mbali hapa nchini.

Alieleza kuwa Italy inajivunia uhusiano wa muda mrefu kati yake na Zanzibar hatua ambayo imepelekea kuimarika kwa uwekezaji katika sekta ya Utalii.

Aidha, Balozi huyo alisema kuwa mbali ya kuimarika kwa sekta hiyo pia, Zanzibar imeweza kupokea watalii wengi kutoka Italy hatua ambayo inatokana na vivutio vilivyopo hapa nchini.

Alisema kuwa wawekezaji walio wengi huvutiwa kuekeza miradi yao katika sehemu ambazo zimewawekea mazingira mazuri ya uwekezaji kama ilivyo kwa Zanzibar.

Balozi Velardi alisema kuwa kutokana na hatua hiyo ipo haja kwa Zanzibar kuimarisha na kuweka mikakati madhubuti kwa wawekezaji wanaokuja kuekeza hapa nchini na kumuhakikishia Rais kuwa wawekezaji kutoka Italy wataendelea kuekeza Zanzibar.

Pamoja na hayo, Balozi huyo alieleza kuwa nchi yake mbali ya kuimarisha uhusiano katika sekta ya uwekezaji, pia, ina mpango wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.

Alisema kuwa tayari kuna mipango maalum imewekwa kwa ajili ya kuleta madaktari kutoa nchini humo kuja kutoa huduma za tiba hapa nchini.

Sambamba na hayo, Balozi huyoa limueleza Dk. Shein kwa niaba yake na Serikali pamoja na wananchi wa Italy wanatoa mkono wa pole kwa wananchi, viongozi wa Zanzibar na Serikali yao kwa msiba mkubwa uliotokea hivi karibuni wa kuzama kwa meli ya MV. Spice Islander.

Nae Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa ujio wa Balozi huyo hapa Zanzibar na kumueleza kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano kati yake na Italy.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Italy ni nchi ya mwanzo iliyoanza kuekeza katika sekta ya Utalii ukiwemo ujenzi wa Hoteli kubwa za Kitalii hapa nchini.

Alisema kuwa Zanzibar imeweza kujitangaza kitaifa na kimataifa katika medali ya kitali ambapo pia, Italy nayo ilichangia kuitangaza Zanzibar kutokana na ujio wa watalii na wawekezaji wengi kutoka nchini humo.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji hasa katika sekta ya utalii kwa kutambua kuwa mchango wa sekta hiyo ni muhimu katika kuimarisha pato la taifa.

Alieleza kuwa mbali ya kuweka mazingira bora ya uwekezaji Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazofuata Utawala Bora hatua ambayo inatoa nafasi kwa wawekezaji wa ndani na nje kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Amesema kuwa Wawekezaji wamekuwa wakifaidika na rasilimali zote ziliopo nchini bila ya kubughudhiwa.

Dk. Shein pia alipokea salamu za rambirambi kutoka serikali na wananchi wa Italy kufuatia msiba huo mkubwa ulioikumba Zanzibar hivi karibuni.

Aidha, Dk. Shein alipongeza nchi hiyo kwa malengo yake ya kupanua zaidi sekta ya uwekezaji hapa nchini sanjari na kuunga mkono sekta ya afya na kueleza kuwa Italy ina histroria ya madaktari wake kutoa huduma za afya hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa Zanzibar ina matumaini makubwa kuwa nchi hiyo itaendeleza uhusiano katika sekta mbali mbali zikiwemo utalii, afya, elimu na nyenginezo.