ISSA MICHUZI AWAPA SOMO LA KUANZISHA BLOGS WASANII


Ankal Michuzi (Issa Michuzi) ambaye ni mmoja wa waasisi wa mitandao ya habari ya jamii (blogs) hapa nchini amewashauri wadau wa sanaa hasa wasanii kuanza kuingia kwa kasi kwenye matumizi ya teknolojia hiyo kwani ni njia kubwa ya kujitangaza na kuuza kazi za sanaa kote duniani.

Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa leo Jumatatu,Michuzi ambaye blog yake ya www.issamichuzi.blogspot.com imepata umaarufu mkubwa kutokana na kutembelewa na watu wengi aliweka wazi kwamba,blogs zimekuwa zikitembelewa na watu mbalimbali duniani hivyo wasanii hawana budi kuzitumia ili kujitangaza, kusambaza kazi zao na hata kujitambulisha katika masoko ya kimataifa.

Alisema kwamba, blogs tofauti na aina nyingine za vyombo vya habari inatumiwa kuhifadhi picha nyingi na kazi mbalimbali, kupata taarifa kuhusu tasnia ya sanaa, kupokea mawazo ya wateja wa kazi za sanaa na hata kuwa na wasaa wa kuwasiliana na wasanii wengine na hivyo kupanuka kimawazo na kiujuzi.

Akizungumzia historia ya blogs,Michuzi alisema kwamba ni teknolojia mpya hapa nchini na kwamba,ilianza kwa kuandika habari za kawaida lakini leo hii ni tegemeo katika kupasha habari kwa uharaka zaidi, kuwafikia watu wengi kuliko vyombo kadhaa vya habari na kimbilio la jamii kwani imekuwa kama sehemu ya jamii katika masuala mbalimbali.

Kwa ujumla Michuzi aliwataka wasanii na wadau wa Sanaa kuamka na kuanza kutumia teknolojia hiyo kwani wasanii mbalimbali duniani si tu wamekuwa wakitumia blog katika kujitangaza na kutambulisha kazi zao bali pia wamekuwa wakimilki mitandao na technolojia mbalimbali za mawasiliano.

Katika kuonesha kwamba, teknolojia hiyo ni muhimu Michuzi ameahidi kuwapa mafunzo ya bure wadau wa Jukwaa la Sanaa juu ya kufungua na kumiliki blog ambayo yataendeshwa Ijumaa ya Desemba 10,2010 kwenye Ukumbi wa BASATA.Wadau wote wa Sanaa mnakaribishwa.