Israel Yasema Itajilinda Kivyovyote Dhidi ya Mashambulizi ya Gaza

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

 

WAKATI mzozo kati ya Hamas na Israel ukizidi kufukuta ukanda wa Gaza, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema nchi yake itachukua kila hatua za kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Gaza. Netanyahu ameyasema hayo leo jioni alipozungumza na waandishi wa habari akizungumzia vitendo vya wanamgambo wa Kipalestina kutoka Gaza.

“Kwa saa 24 zilizopita Israel imeweka sawa kabisa kwamba haitavumilia mashambulizi ya roketi na mabomu yanayofanywa dhidi ya raia wake, natumai Hamas imesikia hilo kama bado Israel iko tayari kuchukua hatua yoyote ile kuwalinda raia wake,” alisema Netanyahu

Netanyahu pia ameelezea kusikitishwa kwake na picha za watoto wa kiisraeli waliouwawa na wengine kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza. Aidha kwa upande wa Palestina kiongozi wa kundi la Hamas Khaled Meshaal ametoa kauli kali dhidi ya Israel akisema wake kwa waume katika mamlaka ya wapalestina wataendelea kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Israel.

Kauli hiyo ameitoa akiwa mjini Khartoum nchini Sudan anakohudhuria mkutano wa makundi ya kiislamu. Halikadhalika rais wa Palestina Mahmoud Abbas amekatiza ziara yake nchini Uswisi kutokana na mgogoro huo unaozidi kutia mashaka.

Hisia mbali mbali zinaendelea kujitokeza juu ya mgogoro huo, Rais wa Misri Mohammed Mursi amelaani vikali mashambulizi yaliofanywa na Israel akisema, huo ni uchokozi unaoanzishwa na Israel katika ukanda wa Gaza. Mursi amesema tayari ameshafanya mazungumzo na rais wa Marekani Barrack Obama juu ya namna ya kusimamisha mzozo huo.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amelaani mashambulizi hayo, huku akiwataka wahusika wote kutojihusisha na mambo ambayo yatawaathiri raia wa kawaida au kusababisha mgogoro zaidi.

“Nasisitiza kwa mara nyingine kwamba jukumu kubwa katika katika mgogoro huu liko mikononi mwa Hamas lakini pia tunaiomba Israel ifanye kila iwezalo kupunguza wasi wasi na kuepuka kushambulia raia na kuongeza matumaini ya uwezekano wa pande zote mbili kuishi kwa amani” alisema waziri Hague.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ametoa mwito kwa viongozi wa pande zote mbili kusimamisha ghasia hizo. Tangu kuanza kwa mashambulizi ya angani ndani ya ukanda wa gaza kutoka Israel takriban wapalestina 15 wakiwemo watoto wawili wameuwawa huku watu wengine 100 wakijeruhiwa. Sasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia Jumuiya ya nchi za kiarabu zinafanya mikutano yao siku ya jumamosi kuzungumzia mgogoro wa Gaza na Israel.

-DW