Islamic State Wamuua Kinyama Mmarekani, Boko Haram Watimuliwa Chibok

Wanamgambo wa Islamic State.

Wanamgambo wa Islamic State.

KANDA moja ya video iliowekwa mtandaoni inaonesha mauaji ya kinyama mfanyakazi wa huduma za misaada raia wa Marekani, Abdul Rahman Kassig ambaye anajulikana kama Peter Kassig kabla ya kutekwa nyara na wanamgambo wa Islamic State nchini Syria mwaka uliopita.

Video hiyo inamuonyesha mawanamume mmoja anayeonekana kuwa mwanachama wa Islamic State akiwa na kisu mkononi na maandishi yanayosema kuwa Peter Kassig ameuawa. Kanda hiyo pia ina picha za watu kadha waliouawa ambao wanasemekana kuwa wanajeshi wa Syria waliokuwa wametekwa nyara.

Marekani imesema kuwa inafanya juhudi za kubaini chimbuko la kanda hiyo. Kassig ambaye anajulikana kama Peter alitekwa nyara mwaka uliopita. Mnamo mwezi Octoba kanda nyengine ya video ya kifo cha mfanyikazi mwengine wa misaada kutoka Uingereza Alan Henning iliisha huku Kassig akitishiwa.

Wakati huo huo; Jeshi la Nigeria linasema kuwa limelikomboa eneo la Chibok siku mbili baada ya wapiganaji Waislamu, Boko Haram, kushambulia mji huo. Wasichana wa shule zaidi ya 200 walitekwa kutoka Chibok mwezi wa Aprili.

Msemaji wa Jeshi, General Olajide Laleye, alieleza kuwa mji umekombolewa lakini alikiri kuwa operesheni bado haikukamilika na inaendelea. Haikuelezwa hasara iliyopatikana. Wapiganaji waliposhambulia Chibok siku ya Alkhamisi, wakaazi waliwashutumu wanajeshi kuwa walikimbia bila ya kupigana.
-BBC