Irente yaiomba Serikali kuchapisha vitabu kwa wenye uono afifu

Warizi Mkuu Mizengo Pinda

JOACHIM MUSHI
Lushoto

SHULE ya msingi ya wanafunzi wasioona ya Irente mjini Lushoto imeitaka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuanza kuchapisha vitabu maalum kwa wanafunzi wenye uwezo mdogo wa kuona.

Changamoto hiyo ilitolewa hivi karibuni na waalimu wa shule ya msingi ya wasioona ya Irente walipokuwa katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi kuzungumzia matatizo kadhaa yanayowakabili wanafuzi wasioona katika shule hiyo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Selina Magambo alisema mbali na shule hiyo kufahamika kama shule ya wanafunzi wasioona wapo baadhi ya wanafunzi wenye uoni afifu ambao kwa sasa hulazimika kutumia vifaa vya kukuza maandishi wanaposoma.

Alisema wanafunzi hao wanauwezo wa kusoma endapo serikali itawatambua na kuanza kuwachapishia vitatu maalumu vyenye maandishi makubwa kulingana na mitaala yao ili waweze kusoma bila vifaa vya kukuzia maneno.

“Wanafunzi hawa wenye uoni afifu wanauwezo wa kusoma kabisa endapo watakuwa na vitabu maalumu vyenye maandishi makubwa tofauti na hivi vinavyotolewa kwa sasa,” alisema Magambo.

Aidha aliongeza kuwa vifaa wanavyotumia kwa sasa ili waweze kusoma kama CCTV za kukuza maandishi na lenzi ni vya gharama za juu kiasi ambacho shule inashindwa kuwa navyo vya kutosha mbali kuwa na gharama nyingine za uendeshaji.

“Mfano CCTV tunazotumia kuwasaidia wanaposoma mbali na kuwa ghali pia zinaendeshwa na umeme kiasi ambacho zinahitaji malipo ya gharama za nishati hiyo kila mwezi mbali na matumizi mengine.. vifaa hivi ni mzigo kwa shule kutokana na gharama,” alisema mwalimu huyo.

Naye, Ofisa Utawala wa shule hiyo, Mshahura Ruben ameitaka wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kupitia viwanda vya uchapishaji vitabu vya wasioona kuhakikisha inaweka utaratibu wa kusimamia uchapishaji na baadae usambazaji kwa shule husika.

Amesema shule za wasioona zimekuwa zikipata tabu kupata vitabu na vifaa vingine vya kufundishia kwa wakati kutokana na urasimu katika zoezi la usambazaji vifaa hivyo.

Alisema kwa sasa shule hizo zimelazimika kusafiri kwa gharama za halmashauri husika mpaka Dar es Salaam kufuatilia vifaa hivyo zoezi ambalo limekuwa likichukua muda kutokana na mlolongo wa utolewaji fedha kutoka katika halmashauri zao.

“Utakuta tunashida na vitabu katika shule yaetu, lakini tutalazimika kuandika barua kwanza halmashauri hapa mnaweza kusubiri zaidi ya wiki mbili ndio mpate fedha na baada ya hapo ndio uanze safari.. mlolongo ambao unapoteza muda wa kufanya shughuli nyingine,” alisema.

Alieleza kuwa endapo viwanda hivyo vingelikuwa vikisambaza vitabu na vifaa hivyo moja kwa moja shuleni kungelikuwa na hauweni kubwa kwa shule hizo na kuondoa urasimu usiokuwa na msingi wowote.