Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kufuta riba yote, ya kiasi cha dola za Marekani milioni 146, ya deni ambalo Iran imekuwa inaidai Tanzania tokea mwaka 1986 kutokana na ununuzi wa mafuta.
Aidha, Serikali hiyo imesema kuwa imekubali pendekezo la Tanzania la kulipa deni la msingi kwa njia za kubadilisha bidhaa na kwa makampuni ya Iran kukaribishwa kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Uamuzi huo wa Serikali ya Iran umetangazwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Reza Rahimi wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, leo, Mei 30, 2012.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, viongozi hao wawili wamezungumzia masuala mbali mbali yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Iran likiwemo deni ambalo Iran imekuwa inaidai Tanzania tokea mwaka 1986 kutokana na ununuzi wa mafuta.
Kuhusu deni hilo, Rahimi amemwambia Rais Kikwete: “Kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, napenda kukujulisha na kutangaza kuwa kuanzia leo Iran imefuta riba yote iliyokuwa imezalishwa kutokana na deni hili.”
Ameongeza: “Iran pia inapenda kukujulisha Rais kuwa iko tayari kuangalia njia mbali mbali za kulipwa deni la msingi ikiwa ni pamoja na nchi zetu mbili kubadilishana bidhaa na makampuni ya Iran kupewa nafasi ya kuwekeza katika uchumi wa Tanzania katika maeneo mbali mbali na hasa kwenye kilimo na afya ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya madawa.”
Rahimi yuko katika ziara ya siku tatu kutembelea Tanzania kwa mwaliko wa Makamu wa Rais, Mohamed Gharib Bilal. Wakati wa ziara yake, kiongozi huyo wa Iran amefanya mazungumzo na viongozi Wakuu wa Tanzania na amefungua ama kuanzisha miradi inayogharimiwa na Iran.
Wakati huo huo, Rais Kikwete leo amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Mjumbe Maalum wa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi. Mara baada ya kupokea ujumbe huo, Rais Kikwete amefanya mazungumzo na Mjumbe huyo, Martin Nivyabandi ambaye ni Waziri wa Maendeleo ya Tarafa (Serikali za Mitaa) wa Burundi.