India Yachangia Maafa ya Kagera sh Milioni 545

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa anatazama mfano wa hundi hiyo na Balozi wa India hapa nchini Sandeep Arya pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa anatazama mfano wa hundi hiyo na Balozi wa India hapa nchini Sandeep Arya pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 27 Septemba, 2016 amepokea msaada wa Shilingi Milioni 545 kutoka kwa Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera waliopatwa na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba, 2016.

Hundi ya fedha hizo imekabidhiwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam na Balozi wa India hapa nchini Mhe. Sandeep Arya na baadaye Rais Magufuli akaikabidhi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

Katika barua yake kwa Rais Magufuli iliyosomwa na Balozi Sandeep Arya, Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi amesema Serikali na Wananchi wa India wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa maafa hayo yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali.

“Tunaziombea amani na uvumilivu familia zote zilizopatwa na madhara na pia tunapenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja na marafiki zetu Serikali ya Tanzania katika kipindi hiki kigumu” amesema Waziri Mkuu Modi.
Kwa Upande wake Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi na Serikali yake kwa kutoa mchango huo na kutuma salamu za rambirambi, na amesema Serikali yake imeguswa na moyo wa upendo waliounesha.

“Mhe. Balozi Sandeep Arya naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu Mhe. Narendra Modi, mwambie kwa niaba ya Serikali yangu tunamshukuru sana kwa kutoa msaada huu muhimu kwa ajili ya Watanzania wenzetu waliopatwa na maafa kule Kagera.

“Mwambie ameonesha moyo wa upendo na ushirikiano kwetu na tumefarijika kwamba marafiki zetu mmeguswa kwa namna ya kipekee na tatizo lililoipata nchi yetu” amesema Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Septemba, 2016