India yaahidi kuisaidia Tanzania teknolojia Rais Kikwete akiwa na mgeni wake, Waziri Mkuu wa India (kulia) Na Joseph Ishengoma – MAELEZO SERIKALI ya India imeahidi kuisaidia Tanzania katika nyanja ya teknolojia ili kuongeza uzalishaji katika mazao ya kilimo. aidha, India imekubali kusaidia uimarishaji wa viwanda vidogo vidogo na kutoa mafunzo ya kitabibu kwa watanzania hasa katika magonjwa ya moyo, kansa na figo. Rais Jakaya Kikwete amewaambia waandishi wa habari Ikulu jijini Dar Es Salaam kuhusu makubaliano ya pande mbili baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu kati Tanzania na ujumbe wa India ulioongozwa na Waziri Mkuu wa wake India Mhe Manmohans Singh. Waziri Mkuu wa India Dr. Singh na ujumbe wake yuko nchini kwa ziara ya siku tatu. “India imekubali kutusaidia katika nyanja ya teknolojia. watatusaidia pia katika kilimo kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kutupatia vifaa vya umwagiliaji katika kilimo kwasababu eneo hili bado halijakua sana ukilinganisha na maeneo mengine,” amesema Rais Kikwete na kuongeza kuwa maendele ya sekta ya kilimo kwa muda mrefu yamekuwa hayaridhishi ikilinganishwa na maeneo mengine kama madini, viwanda na utalii. Sekta ya kilimoo imekuwa ikikua kwa asilimia nne nukta tatu (4.3) wakati ndiyo sekta inayojumuisha idadi nyingi ya watanzania hasa wanaoishi vijijini. Aidha serikali hiyo imekubali kutoa mafunzo ya utabibu wa magonjwa ya moyo, kansa na figo ili kupunguza idadi ya Watanzania wanaokwenda nje ya nchi kupata matibabu ya magonjwa hayo. kwa upande wake Waziri Singh amesema kuwa serikali yake itatoa dola 180 milioni za Kimarekani kuboresha miundombinu ya maji jijini Dar es Salaam. “Tutatoa pia dola za kimarekani milioni 10 kama msaada ili kuwajengea uwezo Watanzania katika mawasiliano ya teknolojia,” amesema. Pande hizo mbili zimesaini mikataba mitatu ya ushirikiano. Mkataba wa kwanza unahusu Shirika la Viwanda vidogo vidogo la Tanzania (SIDO) na Shirika la Taifa la viwanda vidogo vidogo la India, wakati mkataba wa pili ulikuwa kati ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Hospitali ya Apollo ya India kuhusu utoaji wa huduma ya afya na mafunzo kwa matabibu hapa nchini. Hospitali ya Apollo inatarajia kujenga hospitali yake katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. na Mkataba wa mwisho unahusu ushuru wa forodha. baada ya makubaliano hayo, kampuni ya India au ya Tanzania itakayofanya kazi katika nchi mojawapo, itatozwa ushuru mara moja. Waziri Mkuu wa India aliyewasili nchini Mei 26 akitokea nchini Ethiopia, anatarajiwa kuondoka nchini kesho (Mei 28/5/2011)