Inavyoelekea, K.K.K.T. kunafuka moshi…

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya waumini wa makanisa mbalimbali yaliyo chini ya kanisa hilo wamesema hivi sasa kanisa hilo limeingiwa na shetani aliyesababisha mgawanyiko wa makundi mawili, jambo ambalo halimpendezi Mungu na ni hatari katika maadili ya kiroho.

“Kiongozi mzuri hapaswi kulalamikiwa kama maandiko matakatifu yanayosema 1 Timotheo 3:2-7 inamuelekeza askofu mkuu anavyotakiwa kuwa,” amedai muumini mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Muumini huyo amesema hivi sasa waumini katika sharika mbalimbali wamekuwa wakimlalamikia Malasusa kutokana na utendaji wake mbaya hali ambayo imewafanya wengi wao kukimbilia kwenye madhehebu mengine.

“Tuna idadi kamili ya waumini waliohamia madhehebu mbalimbali ambao wote wanadai kuwa hawaridhiki na utendaji wa Malasusa kutokana na mapungufu yake,” amedai muumini huyo.

Ameongeza kuwa kitendo cha Askofu Malasusa kumfukuza mchungaji Enock Mlyuka na Mtheologia wa Kibiti kukataa kubarikiwa na askofu huyo kuwa mchungaji ni dhahiri kuwa anajua mengi juu ya Malasusa ambayo yanamkwaza na kumfanya aone kuwa hapaswi kumuongoza kwenye njia ipasayo.

Ameendelea kudai kuwa katika Usharika wa Azania Front kumekuwa na malalamiko ya watumishi juu ya ucheleweshaji wa mishahara, huku kukiwa na matumizi mabaya ya fedha na watumishi wengine wakijilipa mishahara mikubwa kila mwezi.

“Kitendo cha matumizi mabaya ya fedha kinaweza kuchangia kanisa kuingia kwenye machafuko wakati wahitaji wengi kama yatima wakiendelea kuteseka kwa kukosa misaada inayotolewa na wafadhili wetu,” amesema muumini huyo.

Kutokana na malalamiko hayo, waumini hao wamemuomba Askofu Malasusa kukaa kando ili uchunguzi ufanyike na kupata kiini cha matatizo ndani ya kanisa hilo.

Katika waraka wao ambao gazeti hili limeupata, wamemuomba Naibu Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Ernest Kadiva, kulionea huruma kanisa hilo huku wakizingatia kuwa mishahara wanayojilipa ni sadaka kwa wajane, wazee, watoto na wengi wasio na uwezo.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu malalamiko hayo, Msaidizi wa Askofu, Mchungaji George Fupe, amesema ni kweli kuna malalamiko kutoka kwa waumini na tayari yameanza kufanyiwa kazi.

Askofu huyo amesema si jambo la busara kwa waumini hao kukimbilia kwenye vyombo vya habari kutoa malalamiko yao na badala yake amewaomba kufika Makao Makuu ya kanisa hilo.

Hata hivyo, mchungaji huyo ameahidi kutoa taarifa kamili kuhusu malalamiko hayo.

Hata hivyo, wakati gazeti hili linakwenda mitamboni kulikuwa na taarifa ambazo si rasmi kuwa wachungaji wa kanisa hilo wamepewa waraka wa taarifa mbalimbali zinazolikumba kanisa hilo na kutakiwa kuwaelimisha waumini kuhusu askofu huyo.

source