Na Mwandishi wa EANA, Arusha
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Christine Lagarde ameitahadharisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutofanya haraka katika kutekeleza makubaliano ya Umoja wa Fedha ulitiwa saini hivi karibuni na nchi tano wananchama wa jumuiya hiyo.
Akihutubia jumuiaya ya sekta binafsi nchini Kenya Jumatatu, bosi huyo wa IMF alisema hadhani kwamba EAC iko tayari kwa utekelezaji wa mpango huo na kwamba inahitaji kwanza kushughulikia masuala muhimu ndani ya nchi zao kabla ya kufikia hatua ya kuunganisha fedha zao, kwa mujibu wa habari zilizorushwa na Capital FM Radio ya Kenya.
Lagarde aliwasili Jumapili iliyopita nchini Kenya kwa ziara ya sku tatu nchini humo kujadili uhusiano baina ya IMF na Kenya kwa kukutana na wadau mbalimbali.
Nchi wananchama wa EAC imeshaanza kutekeleza itafaki za Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja na bado hawajaanza kuonja matunda ya hatua hiyo. Hatua ya tatu ni ya Umoja wa Fedha na hatua ya nne na ya mwisho ni Shirikisho la Kisiasa. Miongoni mwa changamoto ambazo mkuu huyo wa IMF amezitaja ni pamoja na kuongzeka kwa vikwazo visivyo vya kodi, tofauti ya uchumi miongoni mwa nchi wanachama na tofauti zilizopo za kodi ndani ya nchi hizo.
“Kama mjumbe wa Umoja wa Fedha wa Ulaya, ninawajibika kuwaeleza kuwa huu ni mradi wenye kuleta hamasi sana, lakini ni mradi ambao Aristotle (mwanafalsafa wa Ugiriki) aliwahi kusema unatakiwa kutekelezwa kwa taratibu. Msiharakishe,” Lagarde alinukuliwa na Capital Radio akisema.
Alisema Kenya ikiwa mstari wa mbele katika kupigia debe mtangamano wa kiuchumi inatakiwa pia kuoongoza wananchama wenzake katika jumuiya hiyo kuhakikisha kwamba makosa yaliyofanywa na jumuiya kama hizo juu ya umoja kama huo, hayarudiwi.
Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo ndiye mwenyekiti wa sasa wa EAC. “Hakikisheni mnajifunza kutokana na makosa yetu na Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki unaweza pia kuwa funzo kwa ule wa Ulaya juu ya kuutekeleza kwa njia iliyo sahihi,” Lagarde alisisitiza.
Itifaki ya Umoja wa Forodha wa EAC ilitiwa saini na wakuu wa nchi wananchama mwezi uliopita mjini Kampala, Uganda, ukiwa umeanzisha rasmimchakato wa kuwa na sarafu moja katika kipindi cha miaka 10 ijayo.