Ilala Yaibwaga Mjini Magaribi Fainali Copa Coca-Cola

Copa Coca Cola

ILALA imepata tiketi ya kucheza fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 upande wa wavulana baada ya kuivua ubingwa Morogoro katika mechi iliyoamriwa kwa mikwaju ya penalti.

Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo uliochezwa leo (Septemba 13 mwaka huu) jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.

Paul Ngowi ndiye aliyeanza kuifungia Ilala dakika ya 30, lakini Morogoro wakasawazisha dakika ya 50 kupitia kwa Omari Sultan. Katika changamoto ya mikwaju ya penalti, Ilala ilipata tatu dhidi ya mbili za Morogoro.

Ilala sasa itacheza fainali na Mjini Magharibi itakayofanyika kesho (Septemba 14 mwaka huu) kuanzia saa 9 alasiri.

Fainali hiyo ya wavulana itatanguliwa na ile ya wasichana kati ya Mwanza na Ilala itakayoanza saa 7 mchana. Mwanza imepata tiketi ya kucheza fainali baada ya leo kushinda nusu fainali ya pili dhidi ya Mbeya kwa mabao 3-0.

Mabao hayo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume yamefungwa na Flora Fulgence dakika ya 47, Emiliana Akuti dakika ya 56 na Yulitha Masamu dakika ya 57.

AIRTEL RISING STARS KUKABIDHIWA BENDERA

TIMU ya Airtel Rising Stars ya Tanzania kwa wavulana na wasichana itakabidhiwa bendera kesho (Septemba 14 mwaka huu) tayari kwa safari ya Nigeria itakayofanyika keshokutwa alfajiri.

Hafla hiyo ya kukabidhi bendera kwa timu hiyo yenye kikosi cha wachezaji 32 itafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah ndiye atakayekabidhi bendera kwa kikosi hicho.

TENGA AWATAKA WAHITIMU GRASSROOTS KUSAMBAZA UJUZI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewataka wahitimu wa kozi ya ukocha wa grassroots kusambaza ujuzi walioupata nje ya shule zao ili mradi huo uwe na manufaa nchi nzima.

Akifunga kozi hiyo iliyoshirikisha makocha 30 kutoka Tanzania Bara na Visiwani kwenye ukumbi wa TFF leo (Septemba 13 mwaka huu), Rais Tenga amewakumbusha kuwa mradi huo umelengwa kuenea nchi nzima katika kipindi cha miaka mitatu.

Mradi wa grassroots unalenga wachezaji mpira wa miguu (wasichana na wavulana) wenye umri kuanzia miaka 6-12, na kozi hiyo ilikuwa chini ya Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Govinder Thandoo kutoka Mauritius.

Washiriki waliohitimu kozi hiyo na kukabidhiwa vyeti ni Abdulkheir Khamis Mohamed (Kaskazini A), Ali Hamad Mohamed (Wete), Ali Khamis Ali (Wete), Amin Amran Yunus (Micheweni), Amina Mhando (Kibaha), Benito Mwakipesile (Kibaha), Deogratius Yesaya (Kibaha), Editha Katabago (Bagamoyo), Habiba Mulungula (Bagamoyo) na Irene Semng’indo (Kibaha).

Juma Omar Abdallah (Kaskazini A), Kassim Ibrahim Mussa (Mkoani), Khamis Haji Ali (Kusini Unguja), Khamis Hamad Rajab (Chakechake), Mahfoudh Abdulla Said (Wete), Marianus Nyalale (Bagamoyo), Maryam Suleiman Ali (Mjini Magharibi), Maryasa Juma Ali (Mjini Magharibi), Mohamed Ali Abdullah (Mjini Magharibi) na Mohamed Salim Omar (Micheweni).

Mohamed Seif Abeid (Mkoani), Ramadhan Kejeli (Bagamoyo), Rhobi Kibacho (Kibaha), Salim Suleiman Juma (Chakechake), Shaaban Naim Suleiman (Kusini Unguja), Shabani Rashid Masimbi (Bagamoyo), Talib Ali Rajab (Chakechake), Thabit Juma Makungu (Kusini Unguja), Yusuf Ali Issa (Mjini Magharibi), Zakia Choum Makame (Mjini Magharibi).

Hiyo ni kozi ya pili ya grassroots kufanyika nchini ambapo ya kwanza ilifanyika Desemba mwaka juzi.

*Imeandaliwa na Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)