Ikulu Yazoa Vikombe SHIMIWI, Wanamichezo Waaswa

Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (waliovalia sare ya bluu) wakisalimiana na wachezaji wa mchezo huo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (waliovalia sare ya rangi ya machungwa) kabla ya mchezo wa robo fainali ambapo timu ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wameibuka washindi na kuingia nusu fainali katika mshindano ya SHIMIWI kwa kuifunga timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu 1- 0.

Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (waliovalia sare ya bluu) wakisalimiana na wachezaji wa mchezo huo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (waliovalia sare ya rangi ya machungwa) kabla ya mchezo wa robo fainali ambapo timu ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wameibuka washindi na kuingia nusu fainali katika mshindano ya SHIMIWI kwa kuifunga timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu 1- 0.


Na Eleuteri Mangi – MAELEZO

KLABU ya Ofisi ya Rais Ikulu imeonesha umwamba wao kwa kupokea vikombe vingi na medali katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamefikia tamati leo mjini Morogoro. Klabu hiyo imeongoza kwa kupokea vikombe vingi zaidi ya klabu nyingine zilizoshiriki michuano hiyo ambapo jumla ya vikombe sita vimechukuliwa na ofisi hiyo kutokana na ufundi wao walioonesha uwanjani katika michezo mbalimbali.

Umwamba huo umeonekana katika mchezo ya kuvuta kamba wanaume ambapo Klabu ya Ofisi ya Rais Ikulu wamekuwa washindi wa kwanza kwa kuwatoa Idara ya Mahakama kwa kuwavuta kwa 2-0 na kwa upande wanawake katika mchezo huo wamekuwa washindi wa pili baada ya RAS Iringa. Katika mchezo wa mpira wa pete (netball), Klabu ya Ofisi ya Rais Ikulu imejinyakulia nafasi ya ushindi wa tatu wakitanguliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nafasi ya pili huku Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma wameshika nafasi ya kwanza katika mchezo huo.

Aidha, vikombe vingine vimetokana na kazi nzuri iliyofanywa katika mchezo wa riadha ambapo Klabu ya Ofisi ya Rais Ikulu imeibuka mshindi wa pili pamoja na mchezo wa karata wanawake. Licha ya Ushindani mkubwa uliojitokeza mwaka huu kutoka timu 54 zilivyojiandaa vizuri kwa mashindano hayo, Klabu ya Ofisi ya Rais Ikulu imepata ushindi huo kutokana na maandalizi mazuri za timu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Mashindano ya SHIMIWI mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu inayosistiza na kuwaalika watumishi wote wa umma kuwa “Michezo ni afya huleta upendo na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi na jamii.”

Wakati huo huo; Wanamichezo nchini wameaswa kuzingatia nidhamu bora ambayo ni msingi wa mafanikio katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamefikia tamati mwishoni mwa wiki mjini Morogoro. Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ikulu Peter Ilomo akimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue wakati wa kufunga mashindano ya SHIMIWI mbele ya umati wa wanamichezo zaidi ya 400 walioshiriki mashindano hayo.
Ilomo amesema amewahimiza wanamichezo kuwa michezo ni afya sio ushindani tu ambapo alibainisha kuwa bila nidhamu mchezaji hawezi kuwa na afya bora yenye tija kwa mtu mwenyewe na katika kutekeleza majukumu yao ya utumishi wa umma. Aidha, Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa Wizara, mikoa, taasisi na Idara za Serikali ziendelee kujitokeza kushiriki mashindano hayo na yachukuliwe kama sehemu ya mahala pa kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera akitoa salamu za mkoa wa Morogoro kwa Mgeni Rasmi amewapongeza wanamichezo wote kwa kushiriki mashindano hayo kwa amani na utulivu ndani ya Manispaa ya Morogoro.
Bendea aliongeza kuwa hadi mwisho wa mashindano hayo, Ofisi yake haijapokea taarifa au malalamiko yeyote yanayoenda kinyume na maadili ya kimichezo.
Hatua hiyo imedhihirisha kuwa wanamichezo wanajua na wamezingatia suala la nidhamu wakati wote wa mashindano hayo kwa kipindi chote cha siku 14 za mashindano kuanzaia Septemba 27 hadi Oktoba 11 mwaka huu. Katika mshindano hayo, timu zilizoonesha nidhamu bora wakati wote wa mashindanoa ndani na nje ya viwanja zimetunukiwa zawadi ya kupewa kikombe kama ishara ya kuwapongeza kwa nidhamu njema. Zawdi hizo zimetolewa kwa wizara, wakala za Serikali na Ofisi za Makatibu Tawala Mikoa (RAS).
Kwa upande wa wizara, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndiyo imekuwa mshindi wa kwanza, ambapo kwa wakala, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMAA) imepokea tuzo hiyo wakati kwa Ofisi za Makatibu Tawala Mikoa (RAS) mkoa wa Lindi ndiyo ulioibuka kidedea. Mashindano ya SHIMIWI mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu inayosistiza na kuwaalika watumishi wote wa umma kuwa “Michezo ni afya huleta upendo na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi na jamii”.