RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameelezea huzuni na masikitiko yake kuomboleza kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mabunge ya Nchi za Jumuia ya Madola (CPA), Dk. William Shija.
Dk. Shija aliyefariki dunia Jumamosi asubuhi mjini London, Uingereza, ambacho ndicho kilikuwa kituo chake cha kazi, alisomea na kuwa mhadhiri wa uandishi wa habari kabla ya kuwa mbunge wa Sengerema kwa miaka 15 mfululizo na Waziri Mwandamizi wa Serikali katika Wizara mbali mbali.
Katika salamu zake kwa Sekretarieti ya CPA, Kanda ya Afrika, Rais Kikwete amesema kuwa amestushwa sana na kifo cha Dkt. Shija ambacho kimeinyang’anya Afrika na dunia, na hasa Tanzania na Jumuia ya Madola, mtumishi mwadilifu na mwaminifu, ambaye alitoa maisha yake kwa utumishi wa umma.
“Alikuwa kiongozi mfano katika nafasi zote za umma alizozishikilia. Aliifanya kazi yake ya uhadhiri wa uandishi wa habari kwa ufanisi mkubwa na aliwapa utumishi uliotukuka wananchi wake wa Sengerema katika nafasi yake ya Ubunge. Dkt. Shija alitumainiwa sana katika nafasi zote nyingi na za uandamizi za Uwaziri wa serikali,” amesema rais Kikwete na kuongeza:
“Nawatumieni salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Dkt. Shija na naungana nanyi katika kumlilia. Kupitia kwenu, nawatumia wajumbe wote wa CPA na Sekretarieti ya Chama hicho pole nyingi sana kwa kuondokewa na kiongozi na mtendaji wao mkuu. Aidha, naomba pia mniwasilishie pole zangu kwa wana-Sengerema ambao Dkt. Shija aliwatumikia kwa uaminifu na kwa miaka mingi.”
“Wajulisheni wote kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa na naomboleza nao na niko nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweka peponi roho ya Marehemu William Shija. Amin.”