RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro kuomboleza vifo vya watu 10 vilivyotokea Mbalizi, Mkoani Mbeya Agosti 29, 2014 baada ya basi dogo la abiria aina ya Toyota Hiace maarufu kama Daladala Na. T 237 BFB kugongana na lori aina ya Tata Na. T 158 CSV. Katika ajali hiyo, watu saba wengine walijeruhiwa na kukimbizwa hospitali kwa matibabu.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 10 na wengine saba kujeruhiwa katika ajali hii iliyotokea siku chache baada ya ajali nyingine kutokea Mkoani Tabora iliyoua watu 19 na wengine 81 kujeruhiwa”, amesema Rais katika salamu zake.
Rais Kikwete amesema mfululizo wa ajali hizi unaonyesha dhahiri kuendelea kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa umakini miongoni mwa madereva, hivyo jitihada zaidi zinatakiwa kufanywa kusimamia kikamilifu Sheria ya Usalama Barabarani na kufuatiliwa kwa karibu kwa mienendo ya wanaoendesha vyombo vya moto, ili ajali hizi ziweze kupunguzwa na hata kudhibitiwa kabisa katika barabara zetu.
“Naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana na ajali hiyo, na kupitia kwako naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa wafiwa wote kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao”Ameongeza.
Rais Kikwete amesema anatambua machungu waliyo nayo wanafamilia, ndugu na jamaa wa watu waliopoteza maisha yao kwenye ajali hiyo, lakini anawaomba wote wawe wavumilivu na wenye subira wakati huu wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao.
“Ninawaombea kwa Mola majeruhi wote wa ajali hiyo waweze kupona haraka na kurejea katika hali zao za kawaida ili waweze kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zao”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika salamu zake.