Ikulu yalionya Gazeti la Dira ya Mtanzania

Bendera ya Rais wa Tanzania

*Ni kwa kudaiwa kulitumia vibaya jina la familia ya JK

GAZETI la kila wiki la Dira ya Mtanzania toleo la leo, Jumatatu, Mei 7, mwaka huu, 2012, limechapisha habari yenye kichwa cha habari, “Familia ya JK yachafuliwa”.
Katika habari hiyo, Gazeti hili linadai kuwa familia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete inafanya biashara na kampuni ya Home Shopping Centre (HSC) ya Dar es Salaam.
Aidha, Gazeti hili linadai kuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Said Saad ndiye msimamizi wa biashara za familia hiyo ya Rais. Tunapenda kuujulisha umma habari hizo si za kweli.
Ni uongo unaolenga kuupotosha umma na kuchafua jina la Rais Kikwete na familia yake, au vinginevyo unalenga kuchafua jina la Kampuni ya Home Shopping Centre. Kama nia ni kufanya hivyo tafadhali msilitumie jina la familia ya Rais.
Rais Kikwete haendeshi, hajawahi kuendesha, na wala hana mpango wa kuendesha biashara iwe ni yeye binafsi au na familia yake. Shughuli azipendazo na ambazo anajishughulisha nazo ni kilimo na ufugaji. Kwa ajili hiyo ana mashamba Sanzale, Kiwanga na Msoga. Hata shughuli hizo hazijafikia kiwango cha kibiashara kwani hutumia pesa yake ya mfukoni kugharamia shughuli hizo.
Badala ya kutoa tuhuma za jumla jumla zisizokuwa na ushahidi wowote ni vema muwe wawazi. Ni vema gazeti likaeleza namna gani au likamtaja ni nani ndani ya familia ya Rais Kikwete anaendesha biashara kwa kushirikiana na Kampuni ya Home Shopping Centre.
Kwa kufanya hivyo, Gazeti la Dira ya Mtanzania litawathibitishia Watanzania kuhusu ukweli wa habari hizo. Aidha, litaondoa doa baya na chafu linalotaka kuelekezwa kwa Rais na Familia yake. Kitendo hicho hakimtendei haki Rais na Familia yake.
Ni imani yetu kuwa Gazeti hili litatoa majibu ya masuala haya muhimu katika toleo lake lijalo, vinginevyo Familia ya Rais itakuwa na haki ya kuchukua hatua stahiki za kisheria.