*Ni kwa wanaodaiwa kumuua Lut. Generali Kombe
Na Mwandishi Wetu
GAZETI la Mwananchi, matoleo ya Jumatano, Oktoba 12 na Oktoba 13, 2011, limeandika habari zilizodai kuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alitoa msamaha wa kupunguza adhabu ya kifo iliyowakabili askari polisi wa zamani waliopatikana na hatia ya kumpiga risasi na kumwua kwa makusudi aliyepata kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe Juni 30, 1996.
Gazeti hili limedai kuwa Rais Kikwete alitoa msamaha huo kwa kupunguza adhabu ya kifo iliyokuwa inawakabili makonstebo wapelelezi Mataba Matiku na Juma Muswa na kuibadilisha kuwa kifungo cha miaka miwili.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kufafanua kuwa Rais Kikwete hajawahi na hajapata kuhusika hata kidogo kutoa msamaha wa kirais kwa kupunguza adhabu ya wauaji hao wa Luteni Jenerali Kombe tokea kuingia madarakani.
Masuala yote yanayohusu polisi hao waliohukumiwa kifo kwa mauaji ya Luteni Jenerali Kombe yalifanyiwa maamuzi kabla ya Rais Kikwete kuingia madarakani Desemba 21, 2005.