Ikulu yakanusha habari ya Tanzania Daima

Bendera ya Rais wa Tanzania

*Yabainisha faida ya ziara ya JK Davos

Na Mwandishi Maalumu

GAZETI la Tanzania Daima la leo, Jumatano, Januari 25, 2012, kwenye ukurasa wake wa kwanza limechapisha habari yenye kichwa cha habari, “Ndege ya JK utata: Iko nje kwa miezi miwili. Serikali yakwama kuilipia.”

Miongoni mwa yaliyoandikwa kwenye habari hiyo ni pamoja na “Ukata unaiokabili Serikali umesababisha kukwama kuilipia ndege hiyo maalum ya Rais…Ndege ya Rais mahususi kwa ajili ya safari za namna hiyo imezuiliwa nje baada ya Serikali kukwama kulipia gharama za matengenezo yake…Kutokuwepo kwa ndege hiyo, kumesababisha Rais Kikwete na ujumbe wake wa watu 14, ulioondoka nchini jana kwenda Davous, nchini Sweden kuhudhuria mkutano wa dunia wa uchumi, kuondoka na ndege ya Shirika la Ndege la Qatal”.

Limeendelea Gazeti hili la Tanzania Daima kudai kuwa kwa sababu ya kutokuwepo kwa ndege hiyo ya Rais gharama za safari hiyo ya Rais zimeongezeka na ziara hiyo ya Rais ya siku nne kuhudhuria mkutano huo itagharimu kiasi cha shilingi milioni 300.

Aidha, Gazeti hili linadai kuwa mkutano huo hauna tija kwa taifa, kwamba Rais Kikwete amehudhuria mikutano hiyo mara nyingi lakini hakuna faida iliyopatikana kwa taifa.

Kwa hakika, maandishi na kauli hizi za ovyo na zisizokuwa za kweli za Gazeti la Tanzania Daima zinalenga kuupotosha umma wa Tanzania bila sababu za msingi na hivyo kuusababishia umma chuki isiyokuwa na msingi kwa Rais. Katika kuuelezea umma ukweli wa safari hiyo ya Rais Kikwete tunapenda kutoka ufafanuzi ufuatao:

Kwanza, kama tulivyoeleza, kwa usahihi, katika taarifa yetu kwa vyombo vya habari jana jioni, Rais Jakaya Kikwete amekwenda katika mji/kijiji cha Davos, nchini Uswisi kuhudhuria Mkutano wa World Economic Forum (WEF) unaoanza leo. Rais Kikwete hakwenda katika mji wa Davous, nchini Sweden kama linavyosema Gazeti hili. Aidha, Rais Kikwete na ujumbe wake umesafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar na siyo Qatal kama linavyoripoti Tanzania Daima.

Pili, Serikali haijakwama, kwa sababu zozote zile, kulipia matengenezo ya kawaida (routine maintenance) ya Ndege ya Rais. Hili limefafanuliwa vizuri na ipasavyo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali, Rubani Kennan Paul Mhaiki jana.

Isipokuwa ni vyema kuongeza kuwa matengenezo ya ndege hiyo yalimalizika Januari 23, mwaka huu, wakati ndege hiyo ilipofanyiwa safari ya majaribio (test flight) kule Savannah, Georgia, Marekani na wala siyo miezi miwili iliyopita kama linavyodai Tanzania Daima. Hivyo, madai kuwa ndege hiyo imezuiliwa nje kwa miezi miwili sasa kwa Serikali kushindwa kulipia gharama za matengenezo ni porojo tu zisizokuwa na msingi.

Tatu, ni vigumu kujua Gazeti la Tanzania Daima limepata wapi habari kuwa safari hiyo ya siku nne inagharimu kiasi cha sh. milioni 300. Ukweli ni safari ya Rais Kikwete na ujumbe wake ni ya siku nane, kama tulivyoeleza jana, ambako atahudhuria mikutano ya WEF na ule wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia atakapowasili Januari 28, 2021. Hivyo, si kweli kwa Gazeti hili kudai kuwa nauli tu na matumizi ya safari ya Rais ni sh. milioni 300 kwa siku nne tu.

Nne, Tanzania Daima linadai kuwa safari za Rais mjini Davos hazina tija na wala faida yoyote. Huu pia ni uongo mwingine wa dhahiri wa Gazeti hili. Tunapenda kukumbusha faida chache tu zilizotokana moja kwa moja na Rais Kikwete kushiriki mikutano ya WEF kama ifuatavyo:

Moja, ni kubuniwa na kupitishwa kwa Mpango Kabambe wa Uendelezaji Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania wa Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) uliozinduliwa wakati wa WEF mwaka jana. Mpango huu utakaotekelezwa kwa pamoja na sekta binafsi na sekta za umma kwa kushirikisha Serikali ya Tanzania, Mashirika ya Kimataifa, Makampuni ya Kimataifa unalenga kuleta faida zifuatazo:

Uwekezaji wa kiasi cha dola za Marekani bilioni 3.4 katika kilimo cha Tanzania na kuongeza uzalishaji wa kilimo hicho mara tatu katika miaka 20 ijayo. Kuchochea uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara kwenye eneo ya hekta 350,000. Kutengeneza kiasi cha ajira 420,000 za kudumu. Kuwatoa kwa namna ya kudumu kiasi cha watu milioni mbili katika umasikini. Kuleta usalama wa kudumu wa chakula kwa kuhakikisha kinapatikana chakula cha kutosha kwa Tanzania na nchi za jirani. Kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, barabara, reli, nishati na bandari katika eneo lote la Mradi wa SAGCOT.
Kuwahakikishia wakulima masoko ya mazao yao, kuwawezesha kupata dhana za kisasa, na kuwaanzishia mifumo ya kisasa ya umwagiliaji.
Kuingizia wakulima mapato ya kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.2 kila mwaka. Kiasi cha dola za Marekani milioni 50 zinaendelea kuingizwa katika mfuko wa uanzishwaji wa Mpango wa SAGCOT utakaotelekezwa kwa kuanzia katika maeneo ya Sumbawanga (Rukwa), Ihemi na Ludewa (Iringa), Kilombero (Morogoro), Mbarali (Mbeya), na Rufiji (Pwani)

Pili, ni uwekezaji kabambe wa kiasi cha dola za Marekani milioni 20 katika mfumo wa upakuaji wa mbolea kwenye Bandari ya Dar es Salaam unaofanywa na Kampuni ya Yara International, moja ya makampuni makubwa zaida ya uzalishaji wa mbolea duniani.

Yara International ni mmoja wa washirika wakubwa katika SAGCOT na uwekezaji wake unalenga kuhakikisha kuwa Tanzania na hata majirani wanapata mbolea ya kutosha kwa ajili ya kuimarisha kilimo.

Tatu, mikutano ya WEF ni shughuli moja inayomwezesha Kiongozi wa Nchi kukutana na kufanya mazungumzo na wakubwa wote duniani – wawe wa siasa, wa biashara, wa uchumi, wa uwekezaji, wa kijamii – katika jitihada zake za kuitangaza Tanzania kama kituo muhimu cha uwekezaji.

Katika siku tatu zijazo, kwa mfano, Kikwete miongoni mwa watu wengine atakutana na Bill Gates wa Bill & Bellinda Foundation, Naibu Waziri wa Uchumi, Nishati na Kilimo wa Marekani, Robert Hormats, Rais wa Benki ya Dunia, Bob Zoellick, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Australia, Kevin Ruud, Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani, Raj Shah, Mtendaji Mkuu wa Benki ya ABSA Bi. Maria Ramos, na Waziri Mkuu wa Thailand Bi. Yingluck Shinawatra.

Tunapenda kumalizia kwa kusisitiza, kwa mara nyingine tena, kuwa ni vyema Gazeti la Tanzania Daima lijiridhishe na usahihi na habari zake kabla ya kuzichapisha kama inavyoelekeza misingi mikuu ya uandishi wa habari na weledi wa kazi hiyo. Uandishi wa habari za uongo unaleta hofu na kuanzisha uzushi usiokuwa na sababu zozote miongoni mwa wananchi na hiyo siyo kazi ya uandishi wa habari.