Ijue Mahakama ya EAC na mafanikio yake

Msajili wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), Profesa John Ruhangisa

MAHAKAMA ya Afrika Mashariki (EACJ) ilitimiza muongo mmoja mwaka jana. Msajili wa Mahakama hiyo Profesa John Ruhangisa amehojiwa hivi karibuni na mwandishi mwandamizi wa Shirika la Habari la Afrika Mashariki (EANA).

Nicodemus Ikonko na kutoa ufafanuzi juu ya shughuli zake kama alivyobainisha katika majibu ya mahojiano hayo.Endelea…

Swali: Mzigo wa kazi za Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) unaonekana kuongezeka hivi karibuni na hivyo kutoa hitaji la Rais wa Mahakama hiyo na Jaji Mfawidhi kuwa na makazi ya kudumu mjini Arusha, makao makuu ya mahakama hiyo. Je maandalizi ya utekelezaji wa adhma hiyo yamekamilika?

Jibu: Taarifa ya tathmini ya utumishi wa majaji wa Mahakama ya Afrika ya Mashariki (EACJ) iliwasilishwa katika mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri, uliofanyika mjini Bujumbura, Burundi kati ya Novemba 21 na 26, 2011. Mkutano huo pamoja na mambo mengine uliagiza kwamba Rais na Jaji Mfawithi wa EACJ wawe ni wakazi wa kudumu mahali ilipo makao makuu ya mahakama hiyo.

Maamuzi hayo pia yaliagiza sekretareti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya mafao ya viongozi hao wakuu wa mahakama hiyo mbele ya kamati ya Fedha na Utawala ili yafikiriwe na kisha yawasilishwe mbele ya Baraza la Mawaziri na hatimaye katika kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Maelekezo hayo yote yamezingatiwa na kwamba kuanzia Julai Mosi, 2012, Rais wa mahakama pamoja na Jaji Mfawidhi watakuwa wakazi wa kudumu makao makuu ya mahakama hiyo mjini Arusha, Tanzania.

Swali: Ni kwa jinsi gani utoaji huduma hiyo ya kudumu ya viongozi hao wawili waandamizi utaongeza kasi ya utendaji kazi wa EACJ?

Jibu: Rais pamoja na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo ambao walikuwa wanatekeleza majukumu yao ya kazi kama wakuu wa idara ya utawala wa chombo hicho na kutoa maagizo ya utendaji kwa kazi wakiwa mbali na makao makuu, sasa wataweza kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi zaidi wakiwa karibu. Ushughulikiaji wa maombi ya dharura yanahitaji maamuzi ya haraka, jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa kabla ya maamuzi hayo, kwa sasa yatashughulikiwa kwa haraka na kwa wakati muafaka.

Swali: Moja kati ya njia za kuhakikisha kwamba mwananchi wa kawaida wa Afrika Mashariki anafahamu uwepo wa mahakama ya EACJ ni kufungua kwa ofisi ndogo za mahakama katika kila nchi mwanachama. Utekelezaji wa jambo hili umefikia hatua gani?

Jibu: Suala la kuanzisha ofisi ndogo za mahakama hiyo liliwasilishwa mbele ya Baraza la Mawaziri, ambalo katika mkutano wake wa Novemba 2011, lilijadili na kupitisha azimio la kuanzishwa kwa ofisi ndogo za mahakama hiyo katika nchi tano wanachama wa EAC. Azimio hilo lilitoa maagizo pia kwamba kila nchi mwanachama za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi, imchague afisa maalum kusimamia shughuli zake.

Baraza pia liliiruhusu mahakama hiyo kuajiri watumishi waliopendekezwa kufanyakazi katika ofisi hizo kwa kuzingatia taratibu za fedha na kuiagiza Sekretarieti ya EAC kuingiza makadirio ya gharama zake katika bajeti ya EAC ya 2012/2013.

Uamuzi huo wa Baraza la Mawaziri na ofisi hizo ndogo, ambazo sasa tayari zimeanza kazi, zitaziduliwa rasmi hivi karibuni. Uzinduzi huo ambao umepangwa kufanyika Agosti 2012, utawawezesha raia kujua uwepo wa ofisi hizo ndogo za mahakama ya EACJ karibu yao..

Swali: Inagharimu kiasi gani kufungua kesi au kuwasilisha malalamiko mbele ya mahakama hiyo ya EACJ?

Majibu: Ni kweli kwamba mahakama hii inadai ada kwa ajili ya kuwasilisha shauri au malalamiko. Viwango vya sasa vya ada ni vya juu kidogo lakini Mahakama hivi sasa inafanyia marekebisho ya kupunguza ada hizo.

Pande husika pia huwaagiza wanasheria wanaowawakilisha katika mashauri yao mbele ya EACJ na kiasi cha ada zinazotozwa kinategemea makubaliano kati ya wakili na mteja husika. Hata hivyo iwapo kuna mgogoro wowote juu ya ada iliyotozwa, suala la namna hiyo linaweza kukatiwa rufaa mbele ya Msajili wa EACJ ili kulitolea uamuzi kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa katika sheria na taratibu zinazotawala mahakama hiyo.

Taratibu za mahakama hiyo zinaruhusu mtu ambaye hana uwezo wa kugharimia ada ya kufungua shauri kuomba asitozwe ada hiyo na hivyo kufungua shauri lake kama mlalamikaji asiye na uwezo wa kulipia gharama hizo.

Swali: Nini mafanikio ya mahakama hii katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita?

Jibu: Kuanzishwa ofisi ndogo katika kila nchi wanachama ni moja ya mafanikio ya mahakama hii na kwamba hatua hiyo itaongeza kujulikana kwa uwepo wake katika kanda nzima. Mahakama imekuwa ikiwahamasisha raia na kusambaza taarifa za shughuli zake kwa umma. Hatua hiyo imeongeza idadi ya kesi zinazosajiliwa katika mahakama hii.

EACJ pia ina ushirikiano na taasisi za mahakama nyingine za kanda ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya, Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya na Mahakama ya SADC.

Pia utekelezaji wa maamuzi ya Rais wa mahakama hiyo pamoja na Jaji Mfawidhi kuwa na makazi yao ya kudumu Arusha ni miongoni pia ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka huo mmoja. Viongozi hao waandamizi sasa wataweza kushughulikia kesi kwa uhakika na ufanisi zaidi.

Swali: Hivi karibuni kulikuwapo na ishara kwamba mamlaka ya EACJ yaongezwe ili kujumuisha kesi zinazohusu pia uhalifu dhidi ya binadamu? Hii ina maana gani katika hali ya kawaida? Hili kweli linawezekana kiufundi na katika hali ya uhalisia wake?

Jibu: Ni kweli kwamba mapendekezo ya kupanua mamlaka ya EACJ yatajumuisha pia makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu na ni kwa mujibu wa maelekezo ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wanaachama. Hii inamaanisha kwamba mahakama hiyo itakuwa na mamlaka ya kushughulikia mashauri kama vile ya mauaji ya kimbari na mengine kama vile ya washukiwa wa Kenya wa uhalifu uliofanywa baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambayo sasa iko mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).

Ingawa mahakama haijafahamishwa au kuhusishwa na jambo hili, ni matarajio yangu kwamba maoni yake yatahitajika katika jambo hili. Vyote, mahakama na Afrika Mashariki kama kanda zina majaji wenye uwezo wa kushughulikia kesi za aina hii. Lakini suala la uwezo wa kuwekeza katika miundombinu yake na rasilimali watu na fedha ni miongoni mwa mambo muhimu yanayohitajika kwa taasisi kama hiyo na ndiyo changamoto kubwa iliyopo ambayo haina budi ishughulikiwe kwanza.

Ili mahakama iweze kushughulikia kesi za aina hii, itahitaji idara mbalimbali zikiwemo za mwendesha mashitaka, upelelezi, usalama wa mashahidi, magereza watakakohifadhiwa washitakiwa wakisubiri kusikilizwa kwa kesi zao na magereza ya kutumikia adhabu zao pindi wakitiwa hatiani. Kiufundi na kiuhalisia inawezekana lakini yapo mambo ya msingi ambayo hayana budi kushughulikiwa kwanza kabla ya kuchukua hatua zaidi juu ya suala hili.

Swali: Tunaweza kusema kwa kujidai kwamba EACJ inaendesha shughuli zake kwa ufanisi na kwa mujibu wa taratibu zake?

Jibu: Ukiyacha matatizo ya kimuundo, kisheria na kimikakati yaliyopo, mahakama hii imefanikiwa kuendesha kazi zake kwa ufanisi. Hata hivyo changamoto nyingi bado zipo kwa siku za usoni za mahakama hiyo.