RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Mei, 2017 amemuapisha Kamishna wa Polisi Simon Nyakoro Sirro kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).
Hafla ya kuapishwa kwa IGP Simon Nyakoro Sirro imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Gerson John Mdemu, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Makatibu Wakuu wa Wizara na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Paul Christian Makonda.
Kabla ya IGP Simon Nyakoro Sirro kuapishwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Mhe. Rais Magufuli amemvua cheo cha zamani cha Kamishna wa Polisi na kumvalisha cheo kipya cha Inspekta Jenerali wa Polisi.
Katika hafla hiyo IGP Simon Nyakoro Sirro, pia amekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Katibu wa Utumishi wa Umma kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. John Marko Kaole. IGP Simon Nyakoro Sirro amechukua nafasi ya Ernest Mangu ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Akizungumza na baadhi ya wanahabari baada ya kuapishwa aliwataka majambazi kuachana na shughuli hiyo aramu kwani atahakikisha wanadhibitiwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria mara moja.