MKUU Mpya wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu ameanza kazi kwa kutangaza mabadiliko ya mfumo wa jeshi hilo huku akiunda vitengo vipya kwa lengo kuongeza ufanisi katika kukabiliana na uhalifu.
Katika mabadiliko hayo, IGP Mangu amesema polisi wameanzisha kamisheni mpya tano ambazo ni Intelijensia, Utawala, Fedha na Ugavi, Upelelezi, Uchunguzi wa Kisayansi wa Kesi za Jinai na Polisi Jamii.
Mfumo huo mpya wa polisi ndiyo uliowezesha kuundwa kwa nafasi mpya ya Naibu IGP, ambayo mteule wake wa kwanza ni Abdulrahman Kaniki ambaye kabla ya hapo alikuwa Kamishna wa Uchunguzi wa Sayansi wa Makosa ya Jinai. Nafasi hiyo sasa inakaimiwa na watu waliokuwa chini yake.
Viongozi wengine katika safu hiyo ni Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Issaya Mngulu, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, Kamishna wa Fedha na Ugavi, Clodwig Mtweve, Kamishna wa Utawala, Thobiasi Andengenye na Kamishna wa Polisi Jamii, Mussa Ali Mussa. Naibu Kamishna wa Polisi, Diwani Athuman yeye anakaimu nafasi ya Kamisheni ya Intelijensia.
Mabadiliko hayo yamekuja wakati Tanzania ikikabiliwa na matukio ya uhalifu ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi wa kiupelelezi, yakiwamo utekaji na utesaji wa watu, ulipuaji mabomu, watu kumwagiwa tindikali, wizi kwa njia ya mitandao na mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mangu alisema amechukua hatua hiyo kutokana na changamoto ya kukabiliana na aina mpya ya uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza katika siku za karibuni. Alifafanua kuwa zamani kazi za Fedha na Ugavi zilikuwa zikifanywa na kitengo cha Utawala na Utumishi.
Mangu alieleza pia kuwa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi ni kitengo kipya katika jeshi hilo.
Alisema mabadiliko hayo yamelenga kuliwezesha jeshi hilo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya sasa.
“Jeshi limepanuliwa kidogo ili kukabiliana na changamoto zilizopo na uteuzi huu ambao pia umefanya kuwapo kwa Naibu IGP kwa mara ya kwanza una maana ya kuongeza ufanisi,” alisema Mangu, akirejea hatua ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Abdulrahman Kaniki kushikilia nafasi hiyo mpya.
Alieleza kuwa wamepewa dhamana ya kuliongoza jeshi hilo kutoka kwa mtangulizi wao, IGP Said Mwema huku kiwango cha uhalifu kikiwa cha wastani na kuahidi kuupunguza maradufu. Alisema wamepokea jeshi hilo tofauti na Mwema, ambaye alipopewa wadhifa huo 2006 kulikuwa na kiwango kikubwa cha uhalifu nchini.
“Tutajitahidi kubuni mbinu mpya za kukabiliana na uhalifu kulingana na mazingira kwani uhalifu kila mwaka unabadilika,” aliongeza Mangu.
Kuchelewesha upelelezi
Mangu alikiri kuwapo kwa tatizo la kuchelewa kwa upelelezi wa kesi zinazohusu uhalifu, ila alijitetea ni kutokana na kujitokeza kwa uhalifu wa aina mpya.
“Tunalazimika kujipanga upya kukabili vitendo vya uhalifu, pia katika masuala ya upelelezi,” alisema na kuongeza kuwa mkakati wao kwa sasa ni kuandaa vijana kwa ajili hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha kutoka serikalini.
“Tunatoa mafunzo kwa vijana jinsi ya kukabiliana na uhalifu mpya kama ule wizi kwa kutumia mtandao,” alisisitiza Mangu.
Pia alizungumzia mapigano baina ya wafugaji na wakulima, ambayo yametapakaa sehemu mbalimbali nchini kama Ifakara, Kilombero na Kiteto.
Polisi na maadili
Mangu alibainisha kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa askari ambao watakiuka sheria na kanuni za jeshi hilo. Alisema atajitahidi na timu yake kuhakikisha hatua zinazofaa zinachukuliwa kwa askari watakaokiuka misingi ya kazi zao na jeshi hilo litaendelea kuwaandaa askari wake kulingana na wakati uliopo.
Pia alizungumzia suala la polisi kutumia nguvu katika kukabiliana na uhalifu na kusema kwamba matumizi ya nguvu itakuwa ni hatua ya mwisho na kwamba itafanyika pale tu watu watakapokaidi amri halali.
“Matumizi ya nguvu ni hatua ya mwisho kwa Jeshi la Polisi hivyo naomba ushirikiano kutoka kwa wananchi na ninawaomba watii sheria bila shuruti,” alisema na kuongeza kuwa yule ambaye anadhani hakutendewa haki kuna njia za kufuata.
Alisema kama sheria ikifuatwa siyo jambo rahisi kwa polisi kutumia nguvu, hivyo kuwataka wananchi kuendelea kutii sheria bila shuruti.
CHANZO: Mwananchi