IDARA ya Habari (MAELEZO) imetakiwa kujipanga vizuri ili kuweza kutekeleza majukumu yake ya kuwa Msemaji wa Serikali ipasavyo; hatua hiyo itasaidia kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na utendaji wa Serikali.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara wakati akifungua kikao kazi cha Maofisa Habari na Mawasiliano wa Serikali katika ukumbi wa Victoria Palace Jijini Mwanza.
Aidha, Dk. Mukangara alisema, Idara ya Habari (MAELEZO) ina jukumu zito la kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali. Hii ni kwa mujibu wa agizo la Serikali Na. C 16 la mwaka 1977.
“Serikali inafanya mambo mengi mazuri kwa wananchi lakini hayasemwi. Matokeo yake Serikali inaishia kulaumiwa na wananchi bila sababu.
“Ndugu zangu hali hii haikubaliki. Lazima tubadilike na lazima tuseme. Hatuwezi kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali asiyesema.”Alisema Dk. Mukangara.
Dk. Mukangara aliongeza kuwa Idara ya habari itekeleze jukumu hilo kwa kushirikiana na Wasemaji wa Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali na Wasemaji hao watambue kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ni Idara ya Habari.
Akizungumzia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari alisema,tunalo tatizo la baadhi ya vyombo vya habari nchini kudhani kwamba uhuru wa vyombo vya habari hauna mipaka. Hivyo alivitaka vyombo vya habari vitambue kuwa hakuna nchi yoyote duniani ambayo utendaji wa vyombo vyake vya habri haubna mipaka.
“Wakati wote uhuru wa vyombo vya habari popote pale huendana na wajibu hata ktika mataifa yaliyoendelea” alisema Dk. Mukangara.
Aidha, alivitaka vyombo vya habari kuwa makini katika kutangaza habari zinazohusu mchakato wa mabadiliko ya katiba huku akisissitiza kuonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kuwahabarisha wananchi na kutoa elimu.
Dk. Mukangara pia aliwataka Maofisa hao kuhakikisha kwamba wanaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa zoezi la Sensa ya watu na Makazi.
Baadhi ya mada zitakazojadiliwa katika kikao hicho cha siku tano chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Sethi Kamuhanda, ni pamoja na Changamoto za utaratibu wa usajili wa magazet; Changamoto zinazoikabili Tanzania katika kuhama kutoka Analojia kwenda Digitali kufikia mwaka 2012; Wajibu wa Maofisa Mawasiliano na mfumo wa mawasiliano Serikalini; na Kazi za Serikali Mtandao na Tovuti kuu.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Monica Mutoni alisema kikao kazi hiki ni fursa kwa Maafisa Habari kuboresha kazi zao na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwahabarisha wananchi majukumu ya Serikali.
Naye Ofisa Habari wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Leonidas Tibanga alisema kuwa baada ya kikao kazi hicho, Maofisa Habari wataweza kupata ujuzi mpya kutokana na mada zitakazotolewa, na kubadilishana uzoefu ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa mawasiliano miongoni mwao.
Vikao kazi vya Maafisa Habari vimekuwa vikifanyika kila mwaka chini ya uratibu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamduni na Michezo ili kujadili namna bora ya utoaji habari za Serikali na uimarishaji wa mawasiliano kwa umma.