Idadi Ya Vifo Vya Mama na Mtoto Barani Afrika Imeanza Kupungua

 

Idadi ya vifo vya Mama na Mtoto barani Afrika imeanza kupungua kutokana na nchi nyingi kufanikiwa katika kupunguza ugonjwa wa malaria ambao nao umekuwa unachangia sana katika vifo vya mama na watoto wachanga barani Afrika.

Rais Jakaya Mrisio Kikwete amesema hayo jana (20 Septemba, 2011) katika mkutano wa viongozi na wadau mbalimbali unaotambuliwa kwa kauli mbiu yake ya “Kila Mwanamke, Kila Mtoto uliofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.

Kuna nchi 11 ambazo zimefanikiwa kupunguza vifo kwa asilimia hamsini (50%) tangu mwaka 2000”. Rais ameeleza na kuonyesha kuwa tangu mwaka 2008, vyandarua vipatavyo milioni 399 vimesambazwa ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa mseto ya Malaria ya Artemisinin (ACT) pamoja na upuliziaji wa dawa za mbu umeongezeka.

Mkutano huu “Every Woman, Every Child” ni mkakati wa kimataifa chini ya Umoja wa Mataifa wenye lengo la kuhamasisha Afya ya Mama na Mtoto kama ilivyoainishwa kwenye malengo makuu ya millennia, ambayo masuala yanayohusu Afya ya Mama na Mtoto ni lengo la 4 na 5  la millennia.

Takwimu zinaonesha kuwa dawa mseto zipatazo milioni 283 zimesambazwa ikiwa ni pamoja na vifaa vya kupimia malaria vimesambazwa katika kipindi cha mwaka 2011.

Pamoja na jitihada hizo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita idadi ya watu waliopata huduma ya kupulizia dawa ya mbu imeongezeka kutoka milioni 10 hadi milioni 70 mwaka huu.

Takwimu pia zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa wa malaria wanaokwenda hospitali imepungua kutoka asilimia 40 hadi asilimia 20 na pia mahudhurio ya shuleni na sehemu za kazi zimeanza kuwa na nafuu.

Rais amezishukuru nchi rafiki na kuziomba kuendelea kutoa mchango na usaidizi wake ili kuziwezesha nchi hizi kuendelea na kuyatunza mafanikio ambayo yameishapatikana.

Mwisho.

Imetolewa na Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,

New York.

Marekani.

21 Septemba, 2011