SAIF al-Islam mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi hajaonekana hadharani tangu mwezi Agosti. Waendesha mashtaka wa kimataifa wamekuwa na “mawasiliano yasiyo rasmi” na mtoto wa kiongozi wa zamani wa .
Mahakama ya uhalifu ya Kimataifa (ICC) imesema watu wa kati wametumika katika mazungumzo hayo yasiyo rasmi na Saif al-Islam.
Taarifa kutoka ndani ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa waendesha mashtaka zinasema mahakama imeweka wazi kwa mtoto huyo wa Gaddafi, kuwa anatakiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, na kuwa hana hatia hadi itakapo thibitishwa mahakamani.
Saif al-Islam, ambaye alidhaniwa kuwa huenda angerithi utawala wa baba yake, amekuwa akijificha kwa miezi kadhaa. Taarifa za hivi karibuni zinadai kuwa alikuwa kwenye msafara unaoelekea kwenye Jangwa la Libya karibu na mpaka na Niger, nchi ambayo washirika wengine wa Gaddafi wamekimbilia.
Lakini taarifa hizo hazijathibitishwa, na ICC imesema haifahamu yuko wapi. Mwendesha Mashtaka wa ICC Luis Moreno Ocampo amesema katika taarifa kuwa ICC inamtaka afikishwe mahakamani.
“Ofisi ya mwendesha mashtaka imeweka wazi kuwa iwapo atajisalimisha kwa ICC, atakuwa na haki ya kesi yake kusikilizwa mahakamani, na hana hatia hadi itakapothibitishwa. Majaji ndio wataamua,” imesema taarifa hiyo. Amri ya ICC ya kukamatwa kwa Saif al-Islam ilitolewa mwezi Juni na inamtuhumu kwa mauaji na utesaji.
Taarifa hiyo inadai kuwa alihusika kwa kiasi kikubwa katika kufanya mashambulio dhidi ya raia katika miji mbalimbali ya Libya, yaliyofanywa na majeshi ya Gaddafi mwezi Februari.
Moreno-Ocampo amesema ICC imefahamishwa kwa “kupitia njia zisiizo rasmi” kuwa mamluki walikuwa wakijitolea kumhamisha Saif al-Islam kwenda katika nchi ambayo haijatia saini makubaliano ya ICC. “Ofisi ya mwendesha mashtaka pia inatazama uwezekano wa kukamata ndege yoyote inayoshukiwa ili kumkamata,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa zinasema huenda Saif al-Islam akaenda Zimbabwe iwapo ataamua kuikimbia ICC. Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe alikuwa mshirika wa muda mrefu wa Muammar Gaddafi. Kiongozi huyo wa zamani wa Libya, ambaye aliiondolewa madarakani mwezi Agosti baada ya miezi sita ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, alikufa kutokana na jeraha la risasi wiki iliyopita baada ya mapigano makali katika jiji la Sirte.
-BBC