ICC yasema mauaji ya Gadaffi ni uhalifu

Marehemu, Kanali Muammar Gaddafi

*Yaanza kuwasaka waliohusika wahukumiwe

KIFO cha aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi ‘kimezua utata’ na kudaiwa kuwa waliohusika kumuua wamefanya uhalifu wa kivita, amesema Kiongozi wa Mkuu wa Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa kuhusu kesi za jinai, Luis Moreno-Ocampo.

Aidha Moreno-Ocampo amesema ICC imeanza kulishuku Baraza la Mseto la Libya (NTC) kuhusiana na uhalifu huo. Kanali Gaddafi aliuawa tarehe 20 Oktoba alipokamatwa na waasi kijijini alikozaliwa Sirte.

Viongozi wa Baraza la mseto mwanzoni walidai kuwa aliuawa wakati wa mapigano, lakini baada ya shinikizo kutoka Mataifa ya magharibi wakasema watafanya uchunguzi.

Moreno-Ocampo amewaambia waandishi wa habari kuwa “nadhani mauaji ya Kanali Gaddafi yanazua maswali na hofu ya uhalifu wa kivita.

“Naona kuwa hili ni suala nyeti. Na tunaelezea hisia zetu kwa wakuu wa nchi hiyo na wao wameanza kuandaa mpango wa jinsi ya kupeleleza uhalifu huu.”

Wapiganaji waasi walimkuta Kanali Gaddafi amefichama ndani ya mtaro wa maji machafu kufuatia mapigano ya muda mrefu yaliyofanyika katika mji alikotoka Kanali Gaddafi wa Sirte.

Picha za video zilizotangazwa wakati wa kukamatwa kwake zilimuonyesha kaueruhiwa ingawa alikuwa hai bado, huku amezungukwa na wapiganaji waasi waliojaa ghadhabu.

Aliburuzwa kupitia halaiki ya watu akipigwa na kuangushwa chini mara kadhaa, kabla ya kupotea huku nyuma yake ikisikika milio ya risasi na mdundo. Mwanae Mutassim, aliyekamatwa naye akiwa hai, aliuawa mikononi mwa waasi hao.

Mahakama ya ICC imemtaja mtoto mwingine wa Kanali Gaddafi, Saif al-Islam, kwa tuhuma za uhalifu katika vita kwa hivi sasa akiwa mikononi mwa Mamlaka ya Libya. Moreno-Ocampo amekubali kuwa kesi dhidi ya Saif al-Islam isikilizwe nchini Libya, na sio The Hague.

-BBC